Sh2.3 bilioni zamtua mama ndoo Moshi

Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa Kija Limbe, akitoa maelezo ya mradi wa maji wa Miwalen Njiapanda kwa kuongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Abdalla Shaib Kaim, wakati mwenge wa Uhuru ulipofika kuzindua mradi huo. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda wenye thamani Sh2.3 bilioni wilayani Moshi, unatajwa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, katika Kata ya Njiapanda wilayani hapo.
Moshi. Kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda wenye thamani Sh2.3 bilioni wilayani Moshi, unatajwa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, katika Kata ya Njiapanda wilayani hapo.
Mradi huo ambao umetekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kwa fedha kutoka Serikalini, umekamilika kwa asilimia 100 huku wananchi wakiwa tayari wameanza kupata huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Muwsa, Kija Limbe wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim alipofika kukagua na kuzindua Mradi huo.
Amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 2,592 kwa siku na kukamilika kwake kumeboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama hata hiyo ya Njiapanda na maeneo jirani ambayo wyalikuwa hayana huduma hiyo kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kabla ya kukamilika kwa mradi huo, upatikanaji wa maji kwenye kata hiyo ulikuwa mita za ujazo 770 kwa siku, huku mahitaji halisi yakiwa mita za ujazo 1,190 kwa siku. Hivyo kukakilika kwake kumemaliza mgao wa maji uliokuwa ukiwakabili wananchi wa maeneo hayo.
"Kukamilika kwa Mradi huu ni ukombozi kwa wananchi wa Kata ya Njiapanda, maana kwa sasa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wanapata maji kwa saa 24, hivyo shughuli za kiuchumi pia zimeimarika kwa kuwa hawapotezi tena muda mrefu kwenda kutafuta huduma ya maji," amesema Mkurugenzi huyo.
Akizindua mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim amesema fedha nyingi za watanzania zimetumika ili kuhakikisha mradi huo wa maji unaleta tija kwa wananchi na kutimiza dhamira ya dhati ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.
"Mwenge wa uhuru umepokea taarifa ya kina inayohusiana na mradi huu wa maji, umefanya ukaguzi wa kina wa nyaraka na kuukagua mradi wenyewe, tumejiridhisha nyaraka zote ziko vuzuri na mradi umezingatia ubora na viwango vinavyohitajika na thamani ya fedha imeonekana hatuna shaka yoyote, tuna matumaini mradi huu unakwenda kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa huduma hii muhimu,” amesema Kiongozi Kaim.
Wakizunguzia mradi huo, baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wamesema kukamilika kwa mradi huo, kumewapa fursa ya kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo na kuboresha kipato chao tofauti na hapo awali ambapo walitumia muda mwingi kusaka huduma hiyo muhimu.
Swaleh Juma amesema awali walikesha wakihangaika kutafuta maji, lakini kwa sasa yanapatikana kwa saa 24, na hivyo kuwawezesha kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo na kuboresha uchumi wao.
"Tuliteseka kwa muda mrefu, watu walihangaika usiku na mchana kutafuta maji hasa kina mama, lakini leo maji yapo ya kutosha na tunaoga muda wote bila wasiwasi, tunaishukuru sana serikali kwa kutufikishia huduma hii muhimu na ya msingi kwetu"amesema Juma.