Wadau waonesha njia kukabili magonjwa ya mlipuko

Muktasari:

  • Wakati magonjwa ya kuambukiza ya kipindupindu na macho mekundu yakiendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali nchini wadau wa na watalaamu wa afya waanisha njia za kujikinga na kuzuia magonjwa hayo.

Dar es Salaam. Wadau na watalaamu wa afya wamependekeza njia mbalimbali zinazopaswa kufuatwa ili kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayojitokeza mara kwa mara kikiwemo kipindupindu kilicholipuka katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza.

Wameeleza hayo leo Jumatano Januari 17, 2024 katika mjadala wa Mwananchi Space uliokuwa na mada ‘tufanye nini kuzuia magonjwa ya mlipuko’ ulioendeshwa na Mwananchi Communications Limited (MCL).

Kati ya Januari 6 hadi 9 ugonjwa wa kipindupindu uligundulika katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza na kuua mtu mmoja, huku watu 98 wakiugua hadi kufikia jana Januari 16, 2024.

Mbali na kipindupindu, ugonjwa wa macho mekundu pia unatajwa kuathiri watu wengi wakiwemo wananchi wa Dar es Salaam, huku Serikali ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Wadau na watalaamu hao wametaja njia hizo kuwa ni kunawa maji safi, kutoa elimu kwa wananchi, kuzingatia usafi, kutambua haraka magonjwa ya aina hiyo.

Mfamasia Tumaini Makole, ameshauri kuimarisha huduma za upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi, akisema mara kadhaa kumekuwa na changamoto ya suala hilo.

“Mara nyingi magonjwa ya mlipuko yanachangiwa na uchafu, lakini pia kuwepo na uhamasishaji wa watu kusafisha mikono yao wanapoenda kupata huduma katika taasisi za umma,” amesema Makole.

Naye, Dk Frank Jacob Matulu kutoka Wizara ya Afya, amesema jambo jingine linalopaswa kufanyika ni kuhakikisha mienendo ya magonjwa ya mlipuko inafuatiliwa ili kuyatambua mapema au kujua ni wakati gani yanaweza kulipuka.

“Mfano kipindupindu akipatikana mgonjwa mmoja sehemu yoyote tayari huo ni mlipuko, cha muhimu ni kuweka mfumo mzuri wa kutambua magonjwa haya yanapojitokeza,” amesema Dk Mafulu.

Dk Mafulu amesema ni vema wananchi wakaelekezwe namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo namna bora, kuepuka ikitokea kuna mgonjwa mmoja ili asimwaambukize mwingine.

“Haimanisha kwamba Wizara ndiyo itambue, bali suala hili lishuke chini hadi katika jamii kuweka mifumo ya utambuzi mapema pindi mgonjwa wa kwanza anapojitokeza ili kuzuia asiambukize mwingine,” amesema Dk Mafulu.

Mbali na hilo, Dk Mafulu amesema kuna vichochoovinavyosababisha magonjwa hayo kuendelea kuwepo katika maeneo mbalimbali akitolea mfano kipindupindu ambacho usipokuwa na majisafi na salama ugonjwa huo kuudhibiti ni changamoto.

“Lakini tuhimize wananchi kunawa mikono iwe wametoka chooni au kutaka kula, pia vyakula vitayarishwe katika chakula katika hali ya usafi na salama,” amesema.

Mdau wa afya, Justin Msengi amesema kunawa mikono ya mara kwa mara, kupeku kushika macho kwa mara kwa mara, sambamba na kusambaza elimu kwa watu mbalimbali hasa mtandaoni, jambo litakalorahisisha watu kupata uelewa kwa haraka zaidi.

“Tunaweza tukatenegeneza matangazo na kusambaza kwa umma kuhusu elimu ya namna bora ya kujikinga na magonjwa haya, lakini pia kutoa elimu kwa vyombo vya habari hasa kutumia watalaamu wa afya,” amesema Msengi.

Mratibu wa Jarida la afya la Mwananchi, Harieth Makwetta akichokoza mada hiyo amesema maeneo yaliyokuwa na ugonjwa mlipuko wa kipindupindu yana changamoto ya usafi.

Amesema katika mkoa wa Mwanza mvua zikinyesha kunakuwa na changamoto ya watu kutiririshaji maji hasa kwa wakazi wanaoishi milimani.

“Hata wanapochimba vyoo wanakutana na mawe, hivyo vinakuwa vifupi kwenda chini, viongozi wanapaswa kuangalia namna gani watatafuta suluhisho la kudumu,” amesema Makwetta.

Makwetta amesema ugonjwa wa kipindupindu unapaswa kuangaliwa kwa jicho jingine, akitolea mfano Nigeria ambako mwaka 2022 wananchi wake zaidi ya 256 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa huo ukisambaa kudhibitiwa kwake kunahitaji nguvu za ziada, akisema katika kipindi cha mwaka 2023 Malawi waliteswa na kipindupindu kutokana na mvua iliyoambatana mafuriko na kusababisha watu zaidi 30,000 kupata maambukizi huku watu 1500 wakipoteza maisha.

Kuhusu ugonjwa wa macho mekundu, Makwetta amesema ulianza taratibu, lakini kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zaidi ya watu 800 wamepata maambukizi baada ya kufika vituo vya afya na kujiandikisha.

“Ugonjwa huu ulianza Dar es Salaam, lakini kwa wiki hii umefika hadi mikoa ya Dodoma, Morogoro na maeneo mengine wagonjwa wameongezeka,” amesema Makwetta.

Makwetta amesema kuna haja ya Serikali kujipanga vema katika kutoa elimu kabla ya majanga ya magonjwa ya mlipuko yasijitokeza mara kwa mara.

Mkazi wa mkoa wa Dar es Salaam, Kalunde Jamal amesema wananchi wana nafasi ya kuzuia magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa kipindupindu, akisema maeneo yanayokuwa na ugonjwa huo yana changamoto zinazoonekana kwa macho.

“Kuna maeneo mengine ukienda tu kwa macho unaona wananchi ndio sababu ya uwepo wa magonjwa hayo, utakuta kuna mrundikano wa taka au utiririshaji wa maji taka lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa,” amesema.

Kalunde amewataka wahusika wakiwemo wakandarasi wa kuzoa taka katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuondoa taka hizo kwa wakati.