Thursday, July 12, 2018

Jinsi gari la wagonjwa lilivyonaswa na mirungi

 

By Beldina Nyakeke, Mwananchi bnyakeke@mwananchi.co.tz

Musoma. Gari la wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime lililotakiwa kusafirisha mgonjwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwenda Bugando jijini Mwanza, limekamatwa likiwa na kilo 800 za mirungi.

Gari hilo, lenye namba DFPA 2955, lilikamatwa jana saa 10 alfajiri wilayani Bunda likipiga ving’ora kana kwamba limebeba mgonjwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema awali dereva wa gari hilo, George Matai, alipigiwa simu akitakiwa kumsafirisha mgonjwa kutoka Hospitali ya Tarime kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando lakini akasema amepata udhuru wa kifamilia na gari hilo halina mafuta.

Akifafanua zaidi Malima alisema baada ya dereva kutoa udhuru, mgonjwa aliyehitaji huduma ya rufaa alisafirishwa kwa kutumia gari la polisi.

“Lakini gari la polisi likiwa njiani kuelekea jijini Mwanza, waliokuwemo ndani ya gari hilo waliiona ‘ambulance’ inayodaiwa kutokuwa na mafuta ikiwa eneo la Bunda, kijiji cha Manyamanyama,” alisema Malima.

“Askari polisi na maofisa wengine waliokuwemo kwenye gari la polisi walilazimika kulisimamisha ili kujua lilikotoka na linakoelekea ndipo wakamkuta dereva ambaye awali alidai gari halina mafuta, ndipo walipokuta limesheheni shehena ya mirungi.” Malima alisema ni aibu kubwa wagonjwa kukosa huduma huku gari likitumika kusafirisha dawa za kulevya.

“Mambo kama haya ndiyo yanatupaka matope Mkoa wa Mara tunaonekana wa hovyo sana, mwananchi anakosa huduma huku rasilimali zikitumika kwenye mambo ya kipuuzi kama haya, hili halivumiliki kamwe lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Mara, Juma Ndaki alisema tayari watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa.

Pamoja na dereva, Kamanda Ndaki aliwataja wengine kuwa ni Luda Joseph, mkazi wa Sirari.

Ndaki alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa shehena hiyo ya dawa za kulevya iliingizwa nchini ikitokea Kenya kupitia mpaka wa Sirari wilayani Tarime.

“Ilikuwa ikipelekwa jijini Mwanza kwa wakala mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi. Wakala huyo husambaza dawa hizo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,” alisema.

Alisema polisi walilikamata gari hilo likipiga king’ora kama limebeba mgonjwa ili kuwalaghai askari wa usalama barabarani wasilikague.

Kamanda Ndaki alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi ili kujua wanaohusika ikiwa ni pamoja na namna ambavyo gari hilo lilitolewa hospitalini na kusafirisha dawa hizo. “Tutawahoji watu wengi akiwamo daktari wa hospitali ya Wilaya ya Tarime ili tujue nani aliruhusu gari kutoka hospitalini na kama kuna uzembe wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Ndaki.

Akizungumzia tukio hilo, kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Innocent Kweka alisema suala hilo lipo mikononi mwa polisi.

“Kuna utaratibu unaotumika kuruhusu magari ya Serikali kutoka, hata mimi suala hili linanisumbua,” alisema Kweka.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga aliiomba polisi kufanya utaratibu ili gari hilo lirudi katika kituo chake cha kazi liendelee kutoa huduma.

“Naliomba Jeshi la Polisi likamilishe taratibu maana hii gari sasa ni kielelezo lakini pia hospitali yetu ina gari moja tu, kwa hiyo ni vyema taratibu zimalizike mapema ili gari lirudi hospitalini likatoe huduma.” alisema Luoga.

Nyongeza na Waitara Meng’anyi.


-->