Theresa atangaza baraza la mawaziri

Muktasari:

Pia amemteua Amber Rudd kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Michael Fallon ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.

London, Uingereza.. Ikiwa ni muda mfupi tu kukabidhiwa funguo za ofisi zilizopo zilizopo mtaa wa Downing nchini Uingereza Thereza May amemteua Boris Johnson kuwa waziri wa Mambo ya Nje pamoja na Philip Hammond kuwa Waziri wa Fedha.

Pia amemteua Amber Rudd kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Michael Fallon ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.

Akizungumza baada ya kupokea ufunguo wa makao rasmi ya waziri mkuu May amehakikishia washirika wake na mataifa ya muungano wa ulaya kuwa licha ya taifa hilo kuamua kujiondoa,Uingereza inapania kujiunga na mataifa shirika na kutekeleza wajibu wake katika muungano wa mataifa huru duniani.

Amesema kuwa serikali yake haitanaswa na mtego wa kuwasikiza mabwenyenye walio wachache na kusahau wananchi wa kawaida.

Theresa May anakuwa  waziri mkuu wa 13 kuwahi kuiongoza Uingereza katika enzi ya Malkia Elizabeth wa pili.

David Cameron amehutubia kwa mara ya mwisho Bunge la Uingereza na kujibu maswali ya wabunge.

Kisha kuwasilisha  barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa Pili katika Kasri la Buckingham.

Malkia  amemtaka mrithi wa Cameron, May kuunda Serikali ikiwa ni historia ya pekee kwa Uingereza kupata kiongozi wa pili mwanamke baada ya Magreth Thatcher.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya  (EU) wameitaka Serikali ya Uingereza kuharakisha mchakato wa kujitoa rasmi katika umoja huo, lakini May amedokeza kuwa hatauharakisha mpango huo mashuhuri kwa jina la Brexit.

Changamoto  kubwa inayomkabili ni pamoja na kuizuia Scotland inayounga mkono Umoja wa Ulaya dhidi ya kuitisha kura ya uhuru wake ili kubakia katika EU na kuimarisha mahusiano mapya ya kibiashara na kidiplomasia ili kujiandaa kwa hali ya baadaye ya baada ya kujiondoa katika umoja huo.