Wazazi lawamani kuchukua baiskeli za wanafunzi za msaada

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akikabidhi baiskeli zilizotolewana Plan Interinational kupitia mradi wa Kagis kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za Wilaya ya Geita.

Muktasari:

 Pamoja na maendeleo ya upatikanaji wa elimu, bado suala la wanafunzi kutomaliza shule ni tatizo


Geita.  Licha ya wanafunzi wa kike kuwezeshwa baiskeli kuhudhuria shule ili wasitembee umbali mrefu, imedaiwa kuwa wazazi na walezi hukwamisha jitihada hizo kwa kuzitumia kinyume na malengo.

Akizungumza wakati akikabidhi baiskeli 550 kwa wanafunzi wa kike leo Ijumaa Aprili 26, 2024 zilizogharimu Sh180 milioni, Mkurugenzi wa Mradi wa Kuwawezesha Wasichana Rika Balehe Kuendelea na Masomo (Kagis)  Mkoa wa Geita, Nicodemus Gachu amesema licha mradi huo kutoa baiskeli hizo kwa walengwa, baadhi ya wazazi na walezi huwapoka na kuzitumia wao.

Shirika la Plan International kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa Canada (GAC), kupitia mradi wa Kagis, limelenga kutoa baiskeli 2,200 kwa wanafunzi wa mikoa ya Kigoma na Geita.

“Baiskeli hizi zinachangia juhudi za Serikali za kuweka mazingira salama, rafiki na wezeshi kwa wasichana walio katika rika balehe ili kuwasaidia kuwahi kufika shuleni, kupata elimu na kuhakiksha kuwa wanabaki shuleni kuendelea na masomo na tunapata wakati mgumu tunapoona lengo hili halitimii kutokana na baadhi ya wazazi au watu wazima kuzitumia kinyume na malengo yetu,” amesema Gachu. 

Amesema pamoja na maendeleo ya upatikanaji wa elimu, bado suala la wanafunzi kutomaliza shule ni tatizo kubwa kwa Mkoa wa Geita na ameiomba Serikali kuangalia kwa undani namna ya kupunguza tatizo hilo.

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi za mwaka 2022 zinaonesha wanafunzi 21,596  wa shule za msingi Geita waliacha shule huku 9,008 wa sekondari wakiacha shule na  kuufanya mkoa huo kuwa wa pili ukiwa na kiwango cha juu cha wanafunzi walioacha shule hapa nchini.

“Tuombe viongozi husika ngazi ya mkoa, wilaya, kata, kijiji, shule kufuatilia matumizi sahihi ya baiskeli hizi ili kuhakisha zinatumika kama ilivyokusudiwa, tunatamani wasichana wanaotembea umbali mrefu na kukutana na vishawishi kwa kuomba lifti wanaondokana na adha hizo,” amesema Gachu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amewataka maofisa elimu kuangalia shule ambazo wanafunzi wamesaidiwa baiskeli.

Pia, amewataka wanafunzi wanaonyang’anywa baiskeli na wazazi au walezi kutoa taarifa kwa walimu ili waweze kuzifuatilia.

“Baiskeli hizi zinagharama kubwa zaidi ya Sh180 milioni, lazima tuone tofauti wakati hatuna baiskeli hali ilikuaje na sasa zimepatikana hali ikoje, wanafunzi kwa wanafunzi lazima nyie muwe mnatoleana taarifa kwa walimu kama mwanafunzi amepewa baiskeli wiki imeisha haonekani shuleni toeni taarifa kwa walimu au viongozi ili tumuone huyo mzazi anayekiuka maagizo haya,” amesema Shigella.

Baadhi ya wanafunzi waliopewa baiskeli hizo akiwamo Elizabeth Emanuel amesema utoaji wa baiskeli utawasaidia kujiendeleza na masomo na kufaulu.

“Baiskeli hizi zitatusaidia sisi wanafunzi tunaoishi mbali tunaweza kufika shule kwa muda muafaka maana huwa tunafika tumechoka uwezo wa kusikiliza unakuwa mdogo,”amesema Emanuel.

Mmoja wa wazazi, Hawa Seth amesema tatizo kubwa halipo kwa kinamama bali kwa kinababa ambao huzitumia kwenda kwenye shughuli zao za kutafuta kipato.