Wazazi wa wanafunzi watoro kukamatwa

Wazazi wa wanafunzi watoro kukamatwa

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Wilson Shimo ameagiza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wanafunzi watoro na wazazi wao ama walezi.

Nyang’hwale. Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Wilson Shimo ameagiza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wanafunzi watoro na wazazi wao ama walezi.

Shimo ametoa agizo hilo juzi, baada ya kubaini kwa kipindi cha mwezi uliopita wanafunzi 56 wa kidato kimoja kwenye Shule ya Sekondari Msalala iliyopo kata ya Kharumwa wilayani humo hawakuhudhuria shuleni.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku zawadi kwa washindi wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020 zilizotolewa kwa walimu, wazazi na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa mwisho, Shimo alisema utoro umekithiri na haukubaliki na unapaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema wakati Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, inasikitisha kuona wazazi ndio wanaochangia wanafunzi kuwa watoro kwa kuwatumia kwenye shughuli za uchimbaji, kilimo na ufugaji.

Akikabidhi tuzo hizo, mrakibu idara ya Mahusiano ya jamii kutoka mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, William Bundala alisema mradi huo unaofadhiliwa na mgodi wao umechangia ongezeko la ufaulu kutoka asilimia 77 mwaka 2019 hadi asilimia 84.7 mwaka 2020.

Alisema mgodi huo ulitenga Sh50 milioni zilizotumika kwa ajili ya kununua vitabu zaidi ya 1,300 na chakula kwa ajili ya wanafunzi wakati wa mchana.

Katibu wa mradi wa kuongeza ufaulu ambaye ni mwalimu wa taaluma kutoka Shule ya Sekondari Msalala, Sulusi Huruma alisema mradi huo ulioanza mwaka 2019 umeongeza ufaulu kwa wanafunzi.