Kimbitor anusa kuwania ubunge Kinondoni

Muktasari:

Kimbitor amepata kura 40 na kuwashinda wagombea wengine sita.

Dar es Salaam. Diwani wa kata ya Hananasifu (Chadema), Ray Kimbitor amepitishwa na mkutano mkuu wa wilaya ya Kinondoni kugombea ubunge jimbo la Kinondoni.

Akitangaza matokeo hayo jana usiku mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Kinondoni, Waziri Muhunzi amesema matokeo hayo watayawasilisha Kamati Kuu Taifa ya chama hicho kwa ajili ya kupata baraka.

Amesema Kimbitor amepata kura 40 na kuwashinda wagombea wengine sita.

Amesema wajumbe wa mkutano huo walikuwa 102 na kura zilizoharibika ni tano.

“Kimbitor amepata kura 40 na kufuatiwa na Mustapher Muro (diwani Kinondoni) aliyepata kura 33,” amesema.

Amesema Rose Moshi amepata kura 5, Nicolas Mkwama kura 16, David Asey kura 2, Moza Ally kura moja huku Juma Uloleulole ambaye ni diwani kata ya Kijitonyama akipata kura sifuri.

Hata hivyo, jana Katibu wa Mambo ya Nje na Itifaki wa Chadema, John Mrema alilieleza Mwananchi kuwa chama kingetoa msimamo huo jana baada ya kuunda kamati ndogo kufanya utafiti, lakini akasema Chadema haikutoa baraka za kufanyika kwa mchakato wa ndani wa kuchukua fomu na kupitisha wagombea.