Nguzo zawaponza mawaziri, RC Hapi, waitwa Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Viongozi wa mkoa wa Iringa wametakiwa kuripoti ofisini kwa Waziri Mkuu kueleza sababu za kuzuia nguzo zisisafirishwe kutoka kwenye halmashauri zao

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi waandamizi wa mkoa wa Iringa akiwemo mkuu wa mkoa huo, Ally Hapi kuripoti ofisini kwake Dodoma saa 5 asubuhi Jumatatu 7, 2019.

Wengine wanaopaswa kuwapo katika kikao hicho ni, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo pamoja na wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za mkoa huo.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana Ijumaa wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga mkoani Ruvuma akisema inashangaza kuona Serikali inafanya jitihada za kusambaza umeme halafu watendaji wa Serikali wanaweka vikwazo.

“Nataka waje waniambie kwa nini wanazuia nguzo, wananchi wanasubiri wao wamezuia nguzo wanasubiri posho wanaidai Serikali na wao Serikali sasa tutakutana ofisini.”

“Yaani sisi tunaahidi umeme uwake kila nyumba ya Mtanzania mpaka yule mnyonge halafu kuna mtu anazuia nguzo na miti hii tumeipanda wenyewe,” amesema.