Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BMH yahitaji Sh17 bilioni kupanua huduma za upandikizaji figo, uboho

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Abdallah Baja.

Muktasari:

  • Hadi sasa hospitali imefanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 56 na uboho kwa watoto 30 waliopona sikoseli. Kampeni ya uchangiaji itafikia kilele Julai 15, ikitarajiwa kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ili kuongeza wigo wa matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji upandikizaji wa figo na uboho kwa watoto wenye ugonjwa wa sikoseli nchini, Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji Sh17 bilioni kufanikisha huduma hizo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Abdallah Baja amesema gharama za upandikizaji wa figo ni Sh45 milioni kwa mgonjwa mmoja, huku upandikizaji wa uboho ukigharimu Sh75 milioni, hali inayowafanya wagonjwa wengi kushindwa kumudu matibabu hayo.

Akizungumza leo, Juni 25, 2026, wakati wa ziara ya wahariri katika hospitali hiyo, Dk Baja amewataka Watanzania kushikamana na kuchangia mfuko maalumu wa kusaidia wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo ili kurejesha matumaini na tabasamu kwao.

“Kuishi ni haki ya kila mtu. Tunaishukuru NHIF kwa mchango wake katika kugharamia matibabu kwa kiwango fulani, lakini bado tunahitaji msaada zaidi kwa wagonjwa hawa,” amesema Dk Baja.

Ameeleza kuwa licha ya Serikali kutoa ruzuku kwa ajili ya matibabu ya magonjwa hayo, fedha hizo bado hazitoshelezi mahitaji kutokana na ongezeko la uhitaji wa huduma hizo nchini.

“Kwa sasa tunaendelea na kampeni ya kuhamasisha jamii kuchangia mfuko huu. Kilele chake kitafanyika Julai 15, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Abdallah Baja (wa pili kulia) akieleza jambo kwa wahariri wakati wa ziara hospitalini hapo leo, Juni 25, 2026.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Dodoma, Irene Kataraihya amesema uchangiaji huo unalenga kuokoa maisha ya Watanzania wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu hayo.

“Matibabu ni gharama, ndiyo maana bima ya afya haikwepeki. Kwa magonjwa haya, mfuko unasaidia kulipia vipimo, dawa na huduma za matibabu baada ya upasuaji,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa bima ya afya, Serikali imetoa Sh48 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kaya zisizo na uwezo ili kusaidia upatikanaji wa huduma za matibabu, ambapo fedha hizo hutolewa kwa awamu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Kitengo cha Figo cha hospitali hiyo, Dk Ayubu Mashambo amesema tangu hospitali ilipoanza kutoa huduma za upandikizaji wa figo mwaka 2020, wagonjwa 56 wamepatiwa huduma hiyo, wakiwamo raia watatu kutoka nje ya nchi.

“Tulianza kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Japan na kutoa huduma kwa wagonjwa 11 mwaka 2020. Kwa sasa huduma hii inatolewa kikamilifu na wataalamu wazawa,” amesema.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya damu, Dk Happiness Igogo amesema hadi sasa watoto 30 wenye ugonjwa wa sikoseli wamefanyiwa upandikizaji wa uboho na kupona ugonjwa huo.

Amesema watoto hao walikuwa na umri kati ya miaka minne na 12 wakati wa kupata matibabu hayo.

“Kutokana na mafanikio ya matibabu ya sikoseli, Tanzania imeanza kutambulika katika Afrika Mashariki na Kati, na tuna dhamira ya kuwa kituo cha umahiri katika matibabu ya ugonjwa huo,” amesema.

Katika ziara hiyo, wahariri walipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya hospitali hiyo, ikiwemo Kitengo cha Upandikizaji Uboho, Kitengo cha Saratani pamoja na dirisha la usajili wa wagonjwa wanaotumia kadi za NHIF.