Bwana harusi afariki dunia akisubiri kufunga ndoa kanisani

Muktasari:

Msiba huo umeibua mjadala mzito katika Jiji la Arusha, lakini zaidi ni upande ule wa bwana na bibi harusi ambako ndugu na jamaa wangali wameshikwa butwaa huku wakijiandaa kwa ajili ya mazishi

Arusha. Sherehe ya harusi iliyokuwa ifanyike juzi jioni katika Kanisa la Nabii wa Utukufu wa Bwana lilipo Olmatejoo, Kata ya Sakina jijini hapa na kwenye ukumbi wa Sariko Olasiti Garden, iligeuka msiba baada ya bwana harusi kufariki dunia ghafla akiwa kanisani.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11 jioni katika kanisa hilo ambapo bwana harusi huyo, Heaven Makupa (47) alikuwa kanisani tangu saa saba mchana akisubiri kufunga ndoa na Jane Kimaro.

Hata hivyo, wakati sherehe, nderemo na vifijo vikiendelea vikiongozwa na kikundi cha matarumbeta nje ya kanisa huku bibi harusi akiingia kanisani, Heaven alianza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.

Kutokana na hali hiyo alikimbizwa Hospitali ya St Elizabeth, lakini alifikishwa akiwa tayari amefariki na mwili wake kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Mhudumu wa chumba hicho, Fransis Costa jana alikiri kuwa wanaendelea kuuhifadhi mwili wa bwana harusi huyo.

Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe na kiongozi wa kanisa hilo, Nabii Peter Alayce na tayari taratibu zote zilikuwa zimekamilika tangu mchana alipofika bwana harusi na ujumbe wake.

Butwaa ukumbini

Wakati kifo hicho kinatokea mamia ya watu walikuwa tayari wamefika katika ukumbi wa Sariko Olasiti Garden kuwasubiri maharusi hao ili kuendelea na sherehe.

Mmoja wa wageni waalikwa, Juliana Mosha alisema kabla ya kifo hicho hakukuwa na taarifa yoyote ya kuugua kwa bwana harusi na walishikiri naye vikao vya harusi hadi dakika ya mwisho. “Hili ni jambo la miujiza, hatujui kilichotokea nadhani hii ni kazi ya Mungu,” alisema Juliana.

Alisema baada ya taarifa kufikishwa ukumbini juu ya msiba huo, watu walianza kutawanyika na kurejea majumbani.

Bibi harusi, taratibu za mazishi

Kutokana na tukio hilo, bibi harusi, Jane, alipatwa na mshtuko ambapo hadi jana baadhi ya ndugu zake ambao hawakupenda kuzungumzia msiba huo walisema alikuwa amepumzishwa.

Akizungumzia na Mwananchi kuhusu mazishi, kaka wa marehemu, Richard Makupa alisema taratibu zinaendelea nyumbani kwa Heaven katika eneo la Kwa Mroboo.

“Hivi sasa tupo kwenye taratibu za msiba, nadhani leo (jana) ndiyo tutapanga siku ya mazishi na mwili bado upo chumba cha kuhifadhi miili Mount Meru Hospital,” alisema.

Nabii aendelea na ibada Jumapili

Wakati majonzi yakitawala katika familia ya bwana na bibi harusi, ibada iliendelea kama kawaida jana kanisani hapo ambapo katika mahuburi yake, Nabii Alayce aliwataka waumini kuishi kwa kumtegemea Mungu.

Alisema Mungu anapowapa uhai na maisha mazuri ni wajibu wao pia kumshukuru kwa kumwabudu.

Nabii huyo alisema imekuwa ni kawaida watu wengi kusahau mambo mema ambayo wanafanyiwa na Mungu, lakini ni vyema wakajua kwamba anawajua.