Chadema na CUF watapinga mswada wa vyama kwa nguvu zote

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji.

Muktasari:

Mashinji amesema Chadema haikubaliani na inapinga muswada huo kwa sababu unalenga kumtengeneza mfalme mpya ndani ya vyama vya siasa

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema muswada wa marekebisho wa sheria ya vyama vya siasa unaondoa uhuru wa kushirikiana kisiasa na kumpa msajili kinga ya kutoshtakiwa au kupingwa katika vyombo mbalimbali vinavyotoa haki.

Ameeleza hayo leo Desemba 9 wakati wa mkutano uliovikutanishwa Vyama 15 vya siasa vya upinzani wakati vikitoa tamko  lao la kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliosomwa bungeni Novemba 16 mwaka huu.

Mashinji amesema Chadema haikubaliani na inapinga muswada huo kwa sababu unalenga kumtengeneza mfalme mpya ndani ya vyama vya siasa.

“Hatukubaliani, muswada huu ni dhaifu, wa hovyo na unalenga kuondoa ushirikiano baina yetu,” amesema

Naibu katibu Mkuu CUF, Joram Bashange amesema sheria hiyo imechukua mapendekezo mengi yaliyofanywa na nchi ya Rwanda 2013 uliompa nguvu Rais wa nchi hiyo Paul Kagame kufanya kile anachokihitaji.

“Hivyo tutapinga kwa nguvu zote kuhakikisha suala hili halifanikiwi ili kuweza kukinga madhara yanayoweza kutokea baadaye na nitashirikiana na mtu yoyote atakayesimama kupinga suala hili,” amesema