Chadema wataka uboreshaji daftari la kupiga kura ufanywe haraka

Mwenyekiti wa kanda ya pwani Chadema, Frederick Sumaye akizngumza na wanahabari

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani leo Jumatatu kimezungumza na waandishi wa habari na kutaka uboreshaji wa daftari la wapiga kura kufanyika haraka ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza huko mbeleni

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kanda ya Pwani kimetaka kufanyika kwa maboresho ya daftari la wapiga kura mapema ili kuepuka zima moto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 24, 2018, Mwenyekiti wa kanda hiyo, Frederick Sumaye amesema kazi hiyo ifanyike kwa muda muafaka na mapema ili baadaye isije kufanyika kwa dharura.

“Tangu uchaguzi ufanyike (mwaka 2015) muda mrefu umepita kuna watu wamekuwa na sifa za kupiga kura, tunaomba kazi hii ya kuboresha daftari kwa kuwaingiza ifanyike mapema,” amesema Sumaye ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu

“Mwakani kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, matumizi ya rasilimali yatakuwa makubwa hivyo basi maboresho yafanyike mapema watu wapate uwezo wa kupiga kura,’’ amesema Sumaye.