Dk Magufuli atimua bosi, avunja bodi Muhimbili

Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli akimjulia hali Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) Dk Helen Kijo Bisimba aliyelazwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam jana baada ya kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea juzi. Picha na Ikulu

Muktasari:

Kidanto anakuwa mtumishi wa kwanza wa umma kukumbana na joto la Rais Magufuli ambaye katika kampeni zake alikuwa akiahidi kwamba akiingia Ikulu, atapambana na watumishi wavivu, wazembe na wasiojisimamia katika kutekeleza majukumu yao.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako alishuhudia utoaji mbovu wa huduma na kuchukua hatua ya kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya hospitali hiyo na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi wake, Dk Hussein Kidanto.

Kidanto anakuwa mtumishi wa kwanza wa umma kukumbana na joto la Rais Magufuli ambaye katika kampeni zake alikuwa akiahidi kwamba akiingia Ikulu, atapambana na watumishi wavivu, wazembe na wasiojisimamia katika kutekeleza majukumu yao.

Hiyo ni ziara ya pili ya kushtukiza aliyofanya Dk Magufuli tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo. Katika ziara ya kwanza alikwenda Wizara ya Fedha na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi. Hata hivyo, wafanyakazi wengi hawakuwapo ofisini wakati huo.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana jioni katika taarifa yake kwamba, Rais alichukizwa na hali aliyoiona Muhimbili ya idadi kubwa ya wagonjwa kulala chini pamoja na mashine za uchunguzi za CT Scan na MRI kuwa hazifanyi kazi kwa miezi miwili sasa wakati hospitali binafsi zikifanya kazi huku wagonjwa wakielekezwa huko.

Alisema Dk Kidanto amerudishwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine. Kutokana na kuondolewa kwake, amemteua Profesa Lawrence Mseru kukaimu nafasi hiyo hadi hapo atakapoamua vinginevyo. Profesa Mseru aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Moi.

Balozi Sefue alisema katika taarifa yake kuwa, Rais ameagiza uongozi mpya kuwa ndani ya wiki moja na zisizidi wiki mbili kuanzia sasa, mashine zote hizo za uchunguzi ziwe zinafanya kazi ipasavyo.

“Kuanzia sasa, baada ya kutengenezwa, anataka kuona mashine hizo zinahudumia wagonjwa wakati wote,” alisema Balozi Sefue.

Alisema jana, Wizara ya Fedha ilitoa Sh3 bilioni kwa ajili ya kutengeneza mashine hizo na za hospitali nyingine nchini ili ziwe zinafanya kazi.

Alisema hospitali hizo zimetakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kufanyia matengenezo pindi mashine hizo zinapoharibika na kuacha kuwa na malimbikizo ya madeni.

Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Taasisi ya Mifupa (Moi) na MNH ili kujionea hali ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini.

Kabla ya kwenda Muhimbili, alimtembelea Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba katika hospitali ya Aga Khan alikolazwa baada ya kupata ajali ya gari juzi, katika makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Akiwa Muhimbili, Dk Magufuli alitembelea pia wodi za Sewa Haji namba 19 na 20, wodi ya wazazi na idara ya huduma za dharura.

Ofisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi alisema Rais Magufuli aliwashukuru wafanyakazi wa Moi na MNH kwa kazi kubwa wanayofanya na uongozi ulimweleza changamoto kubwa hasa ya msongamano wa wagonjwa wodini na upungufu wa vifaatiba.

Almasi alisema kwamba Rais alimjulia hali aliyekuwa mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo aliyelazwa hapo.

Baadhi ya wagonjwa walisema wamefurahishwa na ujio wa Rais Magufuli na kwamba wanaamini ataweza kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya.

Mkazi wa Kitunda, Stella Mwita alisema Rais Magufuli anaweza kazi na lile tatizo sugu la uhaba wa dawa kwenye hospitali za umma litapatiwa ufumbuzi. Alisema huo ni mwanzo mzuri wa utawala wake na anamuombea kwa Mungu afanikiwe katika kazi yake.

“Ndugu yangu amelazwa hapa Sewa Haji, huduma bado siyo nzuri kwa sababu alichelewa kuhudumiwa. Ninaomba Rais wangu ajitahidi kuongeza wauguzi ili wahudumie wagonjwa wengi kwa muda mfupi,” alisema.

Alex Yohana alisema amefarijika kumwona kiongozi wa nchi akitembelea hospitali hiyo na kuamini kwamba amesikia kilio cha siku nyingi cha Watanzania. Alisema akiendelea na kasi hiyo, ataibadilisha nchi hii tofauti na ilivyo sasa.

“Sikumpigia kura Dk Magufuli lakini nimeanza kumkubali kutokana na mambo ambayo ameanza kufanya. Ninatarajia matatizo yote ya hospitali hii na nyingine za Serikali yatatatuliwa baada ya muda mfupi,” alisema Yohana ambaye ni majeruhi wa ajali ya pikipiki.

Samia rasmi ofisini

Katika hatua nyingine; Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana alikabidhiwa rasmi ofisi na Makamu wa Rais mstaafu Dk Mohammed Gharib Bilal, Ikulu.

Baada ya makabidhiano hayo Samia, alikaribishwa na watumishi wa ofisi yake na kuwataka kufanya kazi kwa bidii kulingana na kauli mbiu ya ‘Hapa ni Kazi Tu’.

“Kila mmoja afanye kazi kwa bidii mahala pake pa kazi. Wale ambao kaulimbiu ya Hapa ni Kazi Tu, itawashinda wakae pembeni... watatusamehe”, alisema.