VIDEO: Hiki ndicho walichokisema Mbatia, Cheyo, Rostam Azizi na Shibuda Ikulu

Muktasari:

  • Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, James Mbatia, John Cheyo na John Shibuda pamoja na mfanyabiashara Rostam Azizi leo wamemtembelea Ikulu Rais John Magufuli na kufanya naye mazungumzo

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa, John Shibuda amempongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi alioufanya wa kutatua tatizo la soko la korosho na kumhakikishia vyama vya siasa vinamuunga mkono.

Amesema uongozi wa Rais Magufuli unalenga kurekebisha dosari za mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali na taasisi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa.

Shibuda ambaye ni miongoni mwa viongozi waliokwenda Ikulu jijini Dar es Salaam leo na kuzungumza na Rais Magufuli. Wengine ni John Cheyo, James Mbatia na mfanyabiashara Rostam Aziz.

“Katika miaka mitatu, Rais Magufuli amerejesha sifa ya utaifa wetu ya kuwa nchi ya kuaminika na kusadikika na amekweza ari ya uhuru na kujitegemea.”

“Tulikuwa na hali duni na dumavu ya maendeleo na ustawi wa jamii, tulikuwa na hali ambayo maendeleo yetu hayawiani na maliasili tulizonazo na rasilimali tulizonazo” amesema Shibuda.

Naye Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia amesema katika kutekeleza malengo 17 ya dunia, Tanzania inafanya vizuri katika lengo la elimu ambalo linazungumzia elimu bora na shirikishi.

“Watanzania wote wana kila sababu ya kuendelea kuijenga nchi yao kwa mawazo ya pamoja yanayozingatia ujumbe uliomo katika wimbo wa Taifa unaosisitiza hekima, umoja na Amani,” amesema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo amesema Watanzania wanapaswa kujivunia kuwa na Rais ambaye ameonyesha dhamira njema ya kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Hata kama yatakuwa magumu kiasi gani, akiamua kusema tunakwenda kujenga Stieglers’ Gorge tutakwenda, akiamua kuwa tunakwenda kujenga standard gauge tunakwenda, akiamua watoto watasoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari inafanyika, na katika miaka mitatu hii imedhihirika kuwa maamuzi yake yanalisaidia Taifa sana” amesema Cheyo.

Naye, Mfanyabiashara Rostam Aziz amesema Rais anatengeneza misingi imara ya uchumi unaokua kwa uhakika zaidi kwa kujenga miundombinu ikiwamo barabara, reli na bandari ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira.

“Tunamuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Watanzania tunawekeza katika nchi yetu, kukuza uchumi wetu, hilo ndilo la msingi kwa sisi wafanyabiashara” amesema Rostam Aziz.