Kesi ya mfanyabiashara Akram Aziz yapigwa kalenda

Muktasari:

Kutokana na upelelezi kutokamilika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Akram Azizi hadi 13, 2018

 


Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya  uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Akram Azizi bado haujakamilika.

Aziz anakabiliwa na mashtaka 75 ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na nyara za Serikali, silaha za aina mbali mbali na risasi zake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Elizabeth Shekunde ameeleza hayo  leo Alhamisi Desemba 6, 2018  mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Shekunde amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu  Rwizile baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13, 2018 itakapotajwa tena.

Mshtakiwa huyo anatetewa na wakili Semi Malimi na Alex Mgongolwa.

Katika mashtaka hayo 75, mashtaka mawili ni ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh108milioni, risasi 6,496 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mrajisi wa silaha.

Pia anakabiliwa na shtaka la  kutakatisha Dola 9018, za Marekani, kukutwa na nyama ya Nyati kilo 65 yenye thamani ya Sh4.35milioni bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyama pori.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 30 na 31, 2018 Oysterbay Kinondoni Dar es Salaam.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Aziz  anadaiwa kuwa kati ya Juni na Oktoba 30, 2018 katika eneo la Oysterbay, alijipatia Dola za 9018 za Marekani huku akijua kuwa kiasi hicho cha fedha ni zao la kosa tangulizi la kujihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali pamoja na kukutwa na silaha bila kibali.

Mshtakiwa huyo anaendelea kusota rumande kwa sababu miongoni kwa mashtaka yanayomkabili, likiwemo la utakatishaji fedha halina dhamana.