Kikwete awatunuku wahitimu UDSM, Lowassa aibua shangwe

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akimtunukia digrii ya Uzamivu (PHD) katika mambo ya uwindaji haramu wa wanyama pori Serengeti, Asanterabi Lowassa katika mahafali ya 48 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete leo Jumanne amewatunuku wahitimu 4,742 ya shahada za uzamivu na uzamili pamoja shahada za awali, stashahada na astashahada.

Wahitimu wa elimu ya juu nchini Tanzania wametakiwa kutumia elimu yao kufanya mambo yanayochangia ustawi wa maisha na kuacha yale yanayotishia amani katika jamii.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 13, 2018 na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa William Anangisye katika mahafali ya 48 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Amewataka wahitimu hao kutafuta fursa za ajira badala ya kusubiri fursa ziwafuate.

"Leo hii mnahitimu, ninachowaomba mnapokuwa mnatekeleza majukumu, wajibu wenu mtumie busara, lakini pia muwe na hulka ya kuthubutu kujaribu mambo ambayo yanaonekana ni magumu," amesema Profesa Anangisye.

Katika mahafali hayo wahitimu 4,742 wametunukiwa Shahada za Uzamivu na Uzamili pamoja shahada za awali, Stashahada na Astashahada.

Shahada ya uzamivu wanaume 58 na wanawake 16, Shahada ya umahiri wanaume 280 na wanawake 155, Stashahada ya Uzamili wanaume 8 na wanawake 7.

Shahada za awali wanaume 2,595  na wanawake 1,542.

Wahitimu hao wametunukiwa tuzo hizo na Mkuu wa chuo hicho hicho, Rais mstaafu  Jakaya Kikwete.

Pia, mahafali hayo yamehudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa ambaye aliibua shangwe na vigelegele baada ya kutambulishwa.

Awali, Profesa Anangisye aliwatambulisha wageni mbalimbali waliohudhuria mahafali hayo yaliyofanyika ukumbi wa Mliman City na alipomtambulisha Lowassa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema mwaka 2015, ziliibuka shangwe za kushangilia kutoka kwa wahitimu huku Lowassa mwenyewe akiwapungia mkono.