Magufuli: Siku moja mtanielewa

Rais John Magufuli, akipongezana na Balozi wa Korea nchini, Cho Tae_ick baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja jipya la Selander jijini, Dar es Salaam jana. Kulia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wa kwanza kutoka kushoto ni Spika wa Bunge, Job Ndugai na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Issac Kamwelwe. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Litakuwa na barabara unganishi za kilomita tanoAkizungumzia daraja hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tan-roads), Patrick Mfugale alisema daraja hilo litakuwa na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2.Alisema daraja lenyewe litakalopita baharini, litakuwa na urefu wa kilo-mita 1.03, upana wa mita 20 ambao utakuwa na njia nne za magari.
  • Alisema pia litakuwa na njia za waenda kwa miguu na litakuwa na kingo za pembeni.Alisema daraja hilo litashikil-iwa na nyaya 120 na nguzo zake zitatengenezwa kwa zege. Alisema litakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 180 kwa wakati mmoja na limesanifiwa kuishi miaka 100.
  • “Niwahakikishie watu wanaoishi pembeni ya mradi huo hasa mabalozi kwamba ujenzi utafanyika bila kuathiri nyumba zilizopo kando ya barabara za Toure na Kenyatta. Litajengwa katika hifadhi ya barabara,” alisema Mfugale.Alisema daraja hilo lita-jengwa na mkandarasi kutoka Jamhuri ya Korea, kampuni ya GS Constructors Ltd kwa gharama ya Sh256 bilioni na kati ya fedha hizo, Serikali ya Korea kupitia shirika lake la EOCF itatoa Sh206 bilioni na Serikali ya Tanzania itatoa Sh49 bilioni.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema siku moja Watanzania watamuelewa kutokana na kazi kubwa anayofanya ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa nchini kwa sasa.

Rais alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja jipya la Selander lenye urefu wa kilomita 1.03, litakalokatisha Bahari ya Hindi.

Alisema Serikali imeendelea kufanya jitihada za kuleta mabadiliko nchini kwa kujenga miundombinu mbalimbali kama ya Daraja la Nyerere, flyover ya Mfugale, barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani na ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge na sasa daraja la Selander.

“Haya tunayoyafanya hamuwezi kuelewa leo. Nina uhakika siku za usoni, mtakumbuka. Nina uhakika siku moja mtakumbuka. Mtakumbuka kwamba wapo watu na hasa katika awamu ya tano, walijitahidi kwa ajili ya kuitengeneza nchi hii kwa maendeleo ya Watanzania wote,” alisema.

Aliwataka wananchi wawe wazalendo, wasimamie maadili kama ilivyofanya Korea ambayo alisema miaka ya 1960, ilikuwa na uchumi sawa na Tanzania lakini sasa nchi hiyo imetoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Kuhusu Daraja la Selander

Akizungumzia daraja hilo, Rais Magufuli alipendekeza lipewe jina la Tanzanite ili kutangaza rasilimali za Taifa akisema hiyo itawawezesha hata mabalozi ambao watakuwa wanatumia daraja hilo kutambua kwamba madini hayo yanapatikana Tanzania.

“Mnaweza hata mkaliita Tanzanite Bridge, ninazungumza tu, sijasema mliite hivyo; na hasa kwa kuzingatia kwamba baadhi ya fedha zitakazotolewa hapa zitatokana na mapato ya Tanzanite,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania imekuwa ikipoteza Sh400 bilioni kila mwaka kutokana na msongamano wa magari, hivyo daraja hilo litapunguza msongamano huo na kuokoa kiasi hicho cha fedha.

Alibainisha kwamba daraja hilo litakuwa refu zaidi nchini likiwa na urefu wa kilomita 1.03, likifuatiwa na la Mkapa lenye urefu wa mita 970.5, Daraja la Mto Ruvuma (mita 720), Daraja la Nyerere - Kigamboni (mita 680) na Daraja la Magufuli - Kilombero (mita 384).

Ampa agizo Waziri

Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kufuatilia mapato ya meli iliyonunuliwa na kampuni ya Sinotaship kwa ushirikiano wa Tanzania na China.

Awali, Waziri Kamwelwe alimweleza Rais kwamba katika ushirikiano wa China na Tanzania, ilianzishwa kampuni hiyo ya meli ambayo ilinunua meli 10; kati ya hizo, tano zilipeperusha bendera ya Tanzania wakati tano nyingine zilipeperusha bendera ya China.

“Mpaka sasa nimebaini kwamba meli zote 10 ziliuzwa lakini wamenunua meli moja kubwa ambayo wanasema haiwezi kuja Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu maji yake yana kina kidogo,” alisema Kamwelwe.

Hata hivyo, alisema mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umekamilika katika gati namba moja ambalo sasa linauwezo wa kuipokea meli hiyo kwa sababu ina kina cha mita 15 wakati meli inahitaji kina cha mita 13.

”Nakupongeza Waziri Kamwelwe, umeanza vizuri. Hawa ndiyo mawaziri wabunifu ninaowataka, siyo unakuwa waziri unakaa tu ofisini, unakunywa chai. Sasa nataka ukafuatilie hiyo meli, ujue mapato yake yanakwenda wapi, haiwezekani tukawa na meli lakini hatujui mapato yake yanakwenda wapi,” alisema Rais Magufuli.