Makonda atoa masharti kupokea ndege ya Serikali kesho

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa masharti kwa watu wanaopaswa kujitokeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya mapokezi ya ndege ya Serikali aina ya Airbus A200-300  kesho Ijumaa Januari 11, 2019.


Dar es Salaam. Wakati kesho Ijumaa Januari 11, 2019 Serikali ya Tanzania ikitarajia kupokea ndege yake ya Airbus A200-300, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wanaopaswa kufika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya mapokezi hayo wawe ni aina ya watu wanaotekeleza ahadi zao.

Akizungumza leo Alhamisi Januari 10, 2019 na waandishi wa habari, Makonda amesema ujio wa ndege hiyo umetokana na ahadi za Rais John Magufuli za kulifufua shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

 “Pamoja na changamoto zote hizo za kupingwa, lakini mwanaume huyu (Magufuli)  amekuwa shupavu kapambana na kesho inatua Airbus ya pili ikiwa ni kati ya zile ndege mbili  kubwa alizoziagiza  kati ya ndege saba zinazopaswa kuletwa kwa ajili ya shirika letu la ndege,” amesema.

“Niwaombe tu kama wewe  ni mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na ulishawahi kutoa ahadi ukatekeleza, tukutane kesho Uwanja wa Ndege na wale ambao hawajawahi kutekeleza ahadi zao wasije.”

 “Kwa watakaobaki majumbani tutakuwa tumepata jibu kwamba ni wale ambao wametoa ahadi lakini hawajawahi kutekeleza.”