Mfanyabiashara aliyetuhumiwa kumpa rushwa Lukuvi aachiwa huru

Muktasari:

Leo Jumatatu Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imemwachia huru mfanyabiashara, Mohamed Kiluwa aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kumpa rushwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imemwachia huru mfanyabiashara, Mohamed Kiluwa (50) baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Kiluwa alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kutoa rushwa ya dola za kimarekani 40,000 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Desemba 24, 2018 na Hakimu Mkazi, Samuel Obasi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutolewa hukumu.

"Ushahidi wa upande wa mashtaka umekaa kihisia zaidi, hivyo mahakama yangu imeshindwa kumtia hatiani mshtakiwa, hivyo mahakama hii imemuachia huru Kiluwa" amedai Hakimu Obasi na kuongeza: "Hisia hata kama zina nguvu kiasi gani, haziwezi kufanya mahakama imtie hatiani," amesema Hakimu Obasi.