Mgonjwa wa kwanza kuwekewa figo MNH asimulia aliyoyapitia

Muktasari:

  • Prisca ni mgonjwa wa kwanza kufanyiwa upandikizaji wa figo MNH tangu ilipoanza kutoa huduma hiyo Novemba 21, 2017. Mpaka sasa wag-onjwa 28 wame-shapandikizwa. Kwa sasa anaendelea vizuri, amerejea kazini na anaendelea na maju-kumu ya kufundisha shuleni hapo.

“Mei mwaka jana nikiwa bado kwenye huduma ya kuchujwa damu ‘dialysis’ sitasahau nilitoka kwenye mashine Jumapili bado nasikia kizunguzungu nikasafiri mpaka Morogoro kumzika mama yangu, Jumatatu niliondoka kurudi tena kwenye mashine.”

Hivyo ndivyo anavyoanza kusimulia Prisca Mwingira (31) wakati akizungumza na Mwananchi mjini Morogoro wiki moja iliyopita.

Prisca aliyechangiwa figo na mdogo wake Batholomeo Mwingira (28) na kupandikizwa figo hiyo Novemba 21 mwaka jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema haikuwa rahisi kwake kutambua chanzo cha figo zake kufeli mpaka alipopata tatizo Agosti, mwaka 2016 akiwa katika kituo chake cha kazi Shule ya Sekondari Mikese, Morogoro.

“Nilianza kuvimba mwili na hata nikikaa miguu ilikuwa inavimba na baadaye kuishiwa pumzi, nilipoenda hospitali kupima wakaniambia nina tatizo la figo na lilishafikia hatua ya mwisho,” anasema.

Anasema moja kwa moja alianza kupokea huduma ya kusafishwa damu ijulikanyo kitaalamu kama ‘dialysis’.

“Nilianza kupokea huduma hiyo Septemba, ila nikashangaa tulianza kwa wiki mara moja, ikaja mara mbili kwa wiki baadaye mara tatu, ilibidi mama aulize kulikoni ndiyo akaambiwa mwanao ataishi hivyo mpaka atakapopandikizwa figo nyingine,” anasema.

“Nilipoambiwa natakiwa kufanyiwa ‘dialysis’ mimi na familia yangu tulikuwa hatuelewi ni nini hicho. Baadaye tulifafanuliwa kwamba nitatakiwa kuwekewa ‘cannula’ (kifaa kinachowekwa sehemu ya shingoni ili kupitisha damu kutoka mwilini kwenda kwenye mashine ikiwa ni hatua za kuichuja. Nikashangaa naingizwa theater (chumba cha upasuaji) ilikuwa ngumu kukubali.

“Nikapelekwa wodini, usiku wake nikaambiwa napelekwa kwenye ‘dialysis’, nilidhani labda nitaingia kwenye mashine kisha nitakuwa nimepona kumbe haikuwa hivyo.”

Prisca ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Nanenane iliyopo Morogoro mjini, anasema suala gumu kwake ilikuwa ni kuishi na ‘cannula’ katika shingo yake.

“Unaposafishwa figo lazima uwekewe eneo ambalo mashine itapitia, kwa kawaida utawekewa cannula na miezi mitatu baadaye watabadilisha na kukuwekea fistula mkononi, mimi fistula ilikataa hivyo miezi yote nililazimika kutumia cannula,” anasema.

Kushindwa kulala vizuri, kutokuwa huru ilikuwa ni sehemu ya maisha yake kwani anasema kwa kawaida cannula haitakiwi iingie maji kwa kuwa hilo likitokea ni rahisi kupata maambukizi na kukusababishia homa kali.

“Mimi nilikuwa najitahidi naoga kwa shida na ukiilalia unaweza kusababisha ikachomoka na mwishowe damu zikamwagika,” anasimulia.

Kukaa kwenye mashine ya ‘dialysis’ ni kazi nyingine ambayo Prisca anasema ilisababisha mwili kupata ganzi, “Ukiingia kwenye mashine ukitoka ni kizunguzungu kesho yake hali ikiwa bado haijakaa sawa wala mwili kutengemaa unarudi tena kwenye mashine.”

Maisha kabla ya upandikizaji

Prisca anasema hakuwa katika nafasi nzuri kwani hakuweza kuchangamana na watu na cannula aliyowekewa ilimsumbua muda mwingi.

Anasema huduma ya kusafishwa damu ilimfanya ajisikie kizunguzungu muda mwingi na hivyo kushindwa kuendelea na kazi yake ya kufundisha kwa miezi 15 ya kupatiwa huduma hiyo.

Hakuweza kula vizuri, “Kuna vyakula nilikuwa nikila nauongezea shida mwili kwa sababu tayari figo zote mbili zilikuwa zimefeli, hivyo nililazimika kula vyakula ambavyo vimechujwa sana na baadhi nilikuwa sili kabisa.”

Anasema chipsi, ndizi za aina zote na nyama ya ng’ombe alizuiwa kula na vyakula alivyoruhusiwa ilikuwa kuku na samaki, ugali na wali uliopikwa baada ya kuchujwa.

Chanzo figo kufeli

Baada ya kupata mafunzo kutoka kwa madaktari kwa muda mrefu, Prisca anasema anaamini kwamba chanzo cha figo zake kufeli ni matumizi holela na ya muda mrefu ya dawa za kutuliza maumivu mwilini’.

“Utotoni kitu kilichokuwa kikinisumbua ni vichomi, hivyo kunifanya nimeze dawa hizi...kupunguza maumivu,” alisema na kuonyesha kuwa anaamini zimechangia tatizo lake hilo.