Mtoto anayedaiwa kufungiwa kabatini hatoi sauti

Dodoma. Wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa hali ya mtoto anayedaiwa kufungiwa kabatini kwa miezi mitano, madaktari wametaja tatizo jingine walilolibaini kwa mtoto huyo kuwa hatoi sauti.

Mtoto huyo aliyelazwa wodi ya watoto wenye utapiamlo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, amegundulika kuwa na tatizo la kutotoa sauti hata anapolia, hivyo kuwafanya madaktari kuanza kutafuta sababu.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo jana, Ofisa Muuguzi, Dina Msesa alisema hali ya mtoto huyo inaendelea kuimarika baada ya kumwanzishia lishe ya vyakula vya kuboresha afya yake, lakini tatizo lipo kwenye utoaji wa sauti.

“Mtoto huyu hatoi sauti yoyote wala halii, ila ametulia jambo linalofanya wataalamu waanze kukuna vichwa kutafuta tatizo,” alisema Msesa.

Kuhusu mama wa mtoto huyo ambaye alikuwa mtumishi wa ndani, alisema afya yake imeimarika na mkono uliokuwa umeumia umepona ambapo sasa anaweza kuunyayua tofauti na awali.

Jana, zilizagaa taarifa kuwa msichana huyo na mtoto wake hawapo hospitalini hapo ikidaiwa kuwa wamechukuliwa na wanaharakati na kupelekwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu.

Taarifa hizo zilikanushwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ernest Ibenzi aliyesema binti huyo yupo akiwa anaendelea kupatiwa matibabu pamoja na mwanaye.

“Aondoke aende wapi? Bado yupo hapa anaendelea kupatiwa matibabu na afya yake inaendelea kuimarika,” alisema Dk Ibenzi.

Mwalimu anayedaiwa kumfanyia ukatili msichana huyo bado anashikiliwa na polisi, lakini wanaharakati wanataka afikishwe mahakamani ili haki ijulikane.