Shule binafsi zapigwa marufuku kufukuza wanafunzi wasiolipa ada

Muktasari:

Leo Alhamisi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amezungumza na waandishi wa habari na kupiga marufuku shule binafsi zinazowarejesha nyumbani wanafunzi ambao hawajamaliza ada au michango


Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amepiga marufuku wanafunzi wa shule binafsi ambao hawajamaliza ada kusimamishwa au kufukuzwa shule.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi Januari 10, 2019, jijini Dar es Salaam, Waitara amesema kuanzia kesho Ijumaa ataanza kupokea taarifa kutoka kwa katibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na wadhibiti ubora wa shule ambazo zimewafukuza au kuwarudisha wanafunzi.

Amesema ni marufuku mwanafunzi kusimamishwa au kufukuzwa shule kwa sababu ya kutolipa ada bila kujali anasoma shule ya umma au binafsi.

Waitara amesema jambo jingine ambalo Serikali haikubaliani nalo ni la wazazi kulazimishwa kulipa ada kwa mkupuo na iwapo hawajafanya hivyo wanafunzi hawataendelea na masomo hata kama mwaka uliopita walifanya hivyo.

"Nina sms (ujumbe mfupi wa maandishi) nilizotumiwa na wazazi wa shule ambazo zimerudisha wanafunzi nyumbani kwa kukosa ada na malipo mengine ya kiholela kama vile kulazimishwa kununua sare za shule shuleni, four figure, rim na madaftari ya ganda gumu (counter book),” amesema Waitara.

“Nataka maofisa elimu, wakurugenzi na makatibu tarafa kwenda kwenye hizi shule (anazitaja shule) hadi kufikia kesho niwe na majibu yanayoonyesha kupatikana ufumbuzi."

Waitara pia amewataka wazazi ambao watoto wao wamerudishwa kwa ajili ya kutolipa au kukamilisha ada wafike kwenye ofisi alizozitaja au Tamisemi kwa ajili ya kupatiwa  ufumbuzi.

Naibu waziri huyo amesema kuna haja ya kurudisha mjadala wa ada elekezi.

"Nafanya utaratibu kurudisha mjadala wa kuangalia namna ambavyo Serikali itatoa msimamo wa ada elekezi kwa sababu kuna shule zinatoza kuanzia Sh1.5 milioni hadi Sh6 milioni na zinasema zinatoa huduma," amesema Waitara.

Waitara amefafanua kama mazazi anaweza kulipa fedha yote hiyo kuna haja gani ya kupata mkopo chuo kikuu.

"Hili limekuwa changamoto kwa wanafunzi wengine wanaishi kwa ndugu wanaporudishwa  inazua taharuki kwa wanafunzi na wazazi" amesema.

"Mtoto amesoma shule kwa miaka mitatu na kukamilisha michango yote, anaposhindwa haongezewi hata wiki moja badala yake anafukuzwa shule na mzazi hataki kukanyaga kabisa shule bila kuwa na risiti ya malipo," amesema

"Hili halivumiliki hata kidogo, wakibainika wanaofanya hivyo tutawachukulia hatua kwa sababu wao wanatoa huduma na hawalipi kodi na ninawakumbusha elimu inasimamiwa na Serikali" amesema Waitara