Simulizi ya mwanamke aliyepambana na mamba – 3

Wazazi wa Marita Malambi, Emma Lolensi na Martin Malambi wakiangalia gazeti la Mwananchi lililokuwa na habari ya binti yao aliyejeruhiwa na mamba katika Kijiji cha Dakawa Ukutu, mkoani Morogoro. Marita kwa sasa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI). Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

Leo mwandishi wetu anaelezea mikasa mbalimbali ya watu waliopotea katika katika mto huo na waliojeruhiwa baada ya kushambuliwa na mamba kutoka katika vijiji 18 vinavyopitiwa mto huo.

Katika mfululizo wa makala haya, jana tuliangalia jinsi wasamaria walivyoshiriki kuanzia mwanzo mpaka mwisho katika kumnasua mdomoni mwa mamba, Marita Malambi (25) mwanamke aliyepambana na mamba katika Mto Mgeta huko Dakawa Ukutu na alivyompoteza mtoto wake Godfrey David.

Leo mwandishi wetu anaelezea mikasa mbalimbali ya watu waliopotea katika katika mto huo na waliojeruhiwa baada ya kushambuliwa na mamba kutoka katika vijiji 18 vinavyopitiwa mto huo.

Siyo Marita peke yake

Ni bahati tu kwamba tukio la kushambuliwa kwa Marita liliripotiwa katika vyombo vya habari hivyo kufahamika. Lakini yeye sio wa kwanza wala sio wa mwisho – walikuwapo walioshambuliwa wengine wakapoteza na maisha kabla yake na hata baada ya Februari 17aliposhambuliwa, watu zaidi ya watatu nao wamenusurika kama yeye.

Mmoja kati ya hao alikuwa anaoga na mwingine alikuwa analima pembeni mwa mto huo jioni ya wiki mbili zilizopita.

Makamba anasema matukio mengi ya kushambuliwa na mamba yamekuwa yakiripotiwa zaidi kutokea kati ya saa tisa alasiri mpaka saa 12 jioni.

“Hawa mamba wanatuathiri sana hapa kijijini kwa mfano leo hii kamkosakosa mtu mwingine, wanazagaa sana. Jana pale (anaonyesha pembezoni mwa mto) tumemuona mwingine, hawa mamba ni wengi kina mama wanaanza kuogopa kuteka maji na hata kuogopa kuoga, mto huu inakuwa shida hata kuusogelea. Viongozi wanakuja na matukio wanayajua na tunawaelekeza lakini wanashindwa kuyatatua,” anasema Mlekea.

Kilio kikubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Dakawa Ukutu, Kisaki, Bwakilachini ni hatari ya maisha inayowakabili kutokana na mamba katika mto huo ambao hawana namna ya kuukwepa kutokana na mahitaji yao ya maji na kuvuka.

Lakini pia kuliwa kwa mifugo yao (ng’ombe), wengi wakiyahusisha matukio hayo na mamba, simba na viboko.

Hofu hiyo sio kwa wananchi wa Kijiji cha Dakawa Ukutu peke yao, bali ni pamoja na vijiji jirani ambavyo mto huo umeambaa vikiwamo, Kisaki, Bwakilachini, Sesenga, Milengwelengwe, Mngazi, Bonye na Mbwande.

Rehema Said, mkazi wa Kijiji cha Kisaki anasema watu wanne anaowafahamu hawajulikani walipo na hayo yametokea katika kipindi cha miaka mitano.

“Hawakusafiri lakini wawili waliondoka kwenda mashambani na huko lazima uvuke Mto Mgeta, hawakurudi na hata ilipofuatiliwa bado tulikosa uhakika kama waliliwa na mamba au vinginevyo, tulitafuta miili yao haikupatikana,” anasema.

Anasema licha ya kuwapo kwa wanyama wakali tofautitofauti wanaoweza kujeruhi na kuua binadamu, mamba ni tishio zaidi katika eneo hilo, “Mamba akikukamata anaweza akatafuna kila kitu, ni vigumu kuona masalia.”

Mbali ya Mto Mgeta, kuna mwingine unaoungana na huo wa Kibwaya ambao nao ni tishio kwa watu wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu nao kama za kilimo, ufugaji na hata uwindaji.

“Nimewahi kumuona mamba, hakuwa ananifuata ila nilimuona anaota jua katika njia ambayo nilikuwa nikielekea huko, niliogopa sana na kukimbia. Tangu hapo shamba langu nililitelekeza sijarudi tena,” anasema Mzee Joseph Mwanga, mkazi wa Kisaki.

Juma Mbuga wa Kijiji cha Ukutu anasema kwa kipindi mwaka 2017 na 2018 wamepoteza watu sita ambao walifariki kutokana na kushambuliwa na mamba pembezoni mwa Mto Mgeta.

“Kuna ndugu yetu alikuja kulima bustani akapoteza maisha, mamba alimfuata akamla, mwingine alikuwa anafanya shughuli zake hapa (akionyesha pembezoni mwa mto) akaja kunywa maji mamba akamkamata shingoni, alipiga yowe tukafanikiwa kumfikia na kumpa msaada kwa kumuwahisha kituo cha afya akafia huko.

“Mwanakijiji mwenzetu Abdallah Bila alimpoteza mtoto wake tukaja kumtafuta tukamkuta tayari mamba amemtafuna amemficha chini ya matete tukamchukua na kurudi naye nyumbani tukazika.”

Hata hivyo, Mbuga anasema licha ya masaibu yote hayo, Serikali ya kijiji imekuwa nyuma kuhakikisha inatatua kadhia hiyo inayowakumba kila uchao kwani haionekani kufanya jambo lolote.

“Haifuatilii ipasavyo, tukisema mamba wategwe hawategwi, sasa hatuelewi chochote, tunaomba Serikali ituangalie tunamuomba Rais John Magufuli ajue hili. Sisi ni binadamu na tulipiga kura, lakini viongozi hawatuhudumii tupo kama wanyama, tunakunywa maji machafu, tunahangaika mabomba hakuna watu wote wa kijijini wanakuja kuteka maji katika mto huuhuu, mamba watatumaliza watoto wanaharisha,” analalamika.

Mbogo anasema licha kuwapo kwa changamoto nyingi, anaiomba Serikali ikiangalie kijiji hicho kwani kipo nyuma kimaendeleo.

Mwanaharakati kijiji cha Dakawa Ukutu, Khalfan Chaurembo anasema wanajitahidi kufuatilia changamoto zilizopo kijijini hapo lakini wanashindwa kufikia muafaka kutokana taarifa zao kutoshughulikiwa.

“Maji ni changamoto kubwa lakini tunapokea ahadi nyingi kwamba fedha itatengwa na kauli kama hizo, lakini hakuna kinachofanyika hata msaada ukija hapa kwetu tunarukwa hatujui kwa nini.

“Serikali yetu ya kijiji ingepokea changamoto tunazowapa na kuzisimamia ipasavyo, tungefika mbali lakini tunashindwa kupiga hatua, mamba wanaua wapo, waliokufa wengi tu hawafiki hata hospitali,” anasema Chaurembo.

Anasema mpaka sasa mifugo mingi ikiwamo ng’ombe zaidi ya 500 wa kijiji chake pekee wameliwa katika mto huo lakini hakuna jitihada zinazofanyika kupitia uongozi wa kijiji.

“Tungekuwa na ushirikiano maana kuna taarifa tunatoa, mwaka jana kuna mamba Bwakilachini alikuwa anakamata watu na mifugo, askari walitega kwa nini isiwe hapa kwetu? hata mtu akipotea Serikali yetu hapa kijijini haishtuki kila mmoja anabaki kufanya yake wanaharakati ndiyo tutahangaika,” anasema Chaurembo.

Watu 39 watibiwa Duthumi

Wenyeji wa Kijiji cha Dakawa Ukutu wanasema watu walioshambuliwa na mamba na wakapatikana hai na kutibiwa ni wachache, wengi wao wamekuwa wakiopolewa wakiwa tayari wamefariki au kupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini hivyo kurudishwa nyumbani na kuzikwa hivyo taarifa zao hazirekodiwi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Duthumi, Dk Kazimili Subi anasema wamekuwa wakipokea majeruhi walioshambuliwa na mamba na kuwatibu kwa nyakati tofauti.

“Tunazo takwimu za miaka mitatu, mwaka 2016 tulikuwa na kesi 23 za wagonjwa waliofikishwa hapa wakiwa wamekamatwa na mamba na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wakubwa kwa watoto. Mwaka 2017 zilipungua kidogo tukawa na kesi kama hizo 13 hivi na mwaka huu hii ni kesi ya tatu kwa sababu mvua kidogo zimechelewa, zikianza kukolea tu majeruhi tunalaza hata wawili au watatu,” anasema Dk Subi.

Dk Subi anasema kituo hicho kimekuwa kikitunza dawa za antibiotiki kwa wingi ili kutibu wagonjwa wa ajali ya kuvamiwa na mamba ambao hujitokeza mara kwa mara.

“Tulipompokea Marita Februari 17, tukampatia dawa za antibiotiki za hali ya juu kwa ajili ya kumuandaa kumpeleka hospitali ya mkoa na dawa tulizompa ni metranidazole na dawa za maumivu kisha tulimpumzisha kwa ajili ya kusubiri kumpatia rufaa,” anasema.

Wagonjwa waliojeruhiwa na mamba wanakuwa wengi wakati wa mvua, ambao maji yanakuwa mengi, “Mwaka jana kuna mtu alikamatwa na mamba njiani kwenye njia ya kawaida, maji yalikuwa kwenye urefu wa magoti, yule mama alikuwa jasiri akapambana naye na kumshinda hakuvunjika ila aling’atwa kwenye paja akachanwa chanwa mwilini wakati akipambana naye aliletwa hapa tulimtibu kwa antibiotiki na kumshona majeraha ya mkono, baadaye tulimruhusu.”

Anasema kutokana na mamba kula mizoga wana bakteria hivyo lazima wanaoshambuliwa wapewe dawa hasa za tetanasi, antibiotiki kwa saa 24 dozi ambayo mgonjwa hulazimika kuimaliza ili awe sawa kwani inazuia wadudu kuzaliana.

“Kama si wa kumpa rufaa basi tutamruhusu. Tunakuwa tumeingilia au tumekatiza maambukizo ambayo yanakwenda kukifanya kidonda kioze au kitoe usaha,” anasema Dk Subi.

Haya yote yametokana na kukosekana kwa huduma za maji kwa wananchi wa eneo hilo. Lakini je, nini mtazamo wa Serikali ya kijiji kuhusu masaibu ya mamba hao na hatua gani imechukua ili kuhakikisha inatatua kero ya upatikanaji wa maji.

Ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Morogoro na ile ya maliasili wanazungumza nini kuhusu mamba hao? Fuatana na mwandishi wetu katika mfululizo wa ripoti hii.

ITAENDELEA KESHO