Watano waripotiwa kufa maji, miili yao yapatikana Mombasa

Muktasari:

Ni wananchi 11 waliokuwa wakisafiri kutoka Zanzibar kwenda Pangani kwa njia ya bahari.

Tanga. Wananchi watano wamefariki dunia huku wengine sita wakijeruhiwa, baada ya boti yao iliyokuwa ikitokea Zanzibar kwenda Wilaya ya Pangani mkoani Tanga,  kupotea baharini tangu juzi Mei 4, 2024 na miili yao kupatikana  Mombasa nchini Kenya.

Leo, Mei 6, 2024, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah amethibitisha kutokea kwa tukio hilo,  lililomfanya aahirishe ziara yake katika Wilaya ya Pangani,  huku akieleza kwamba watu watano kati ya 11 waliokuwa kwenye boti hiyo wamepatikana wakiwa wamekufa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi,  amelieleza Mwananchi kwa njia ya simu kwamba hana taarifa kuhusiana na tukio hilo, hivyo na yeye anafuatilia ili kupata undani wa taarifa hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mussa Kilakala amesema  atatoa taarifa kuhusiana na suala hilo.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Tanga, amesema wananchi hao wameonekana wote, lakini watano kati yao wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa, hivyo taratibu za kurudisha miili ya marehemu na majeruhi zinafanyika na ubalozi mdogo wa Tanzania uliopo Mombasa.

Amesema katika kundi hilo la watu 11, walikuwemo wafanyabiashara ambao ni wajasiriamali pamoja na raia wa kawaida, ambao walikuwa wakisafiri na boti hiyo kutoka Zanzibar kwenda Pangani.

Jana usiku, taarifa zilitolewa kwamba mwenyekiti huyo ameahirisha ziara yake katika Wilaya ya Pangani iliyotakiwa kuanza leo kutokana na kuwepo taarifa za wananchi 11 kupotelea baharini.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa tangu juzi wananchi hao walikuwa wakitafutwa lakini hakukuwa na mafanikio na haijulikani kama wako hai au wamefariki, na juhudi za kuwatafuta zilikuwa zikiendelea katika pwani ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

“Mei 6, 2024 tulikuwa tufanye mkutano kwenye kata ya Madanga, Wilaya ya Pangani, lakini tumeahirisha kwa huzuni kubwa ya ndugu zetu wa Pangani 11 tangu juzi hadi leo hatujafanikiwa kuwapata wakiwa hai au wamefariki.

“Jitihada za kuwatafuta zinaendelea pwani yote ya Bahari ya Hindi na nchi jirani,” alisema sehemu ya taarifa hiyo ya Mwenyekiti Rajabu.