Wanafunzi walivyonusurika kufa maji Arusha

Muktasari:

  • Wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial wafariki, msamaria mwema mmoja.

Dar es Salaam. Wanafunzi walionusurika katika ajali iliyoua wenzao saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial, jijini Arusha wamesimulia ilivyotokea, wakieleza kuwa dereva alidharau ushauri wa matroni wao.

Ajali hiyo imetokea leo Aprili 12, 2024, wakati gari la shule hiyo iliyoko eneo la Murieti, likiwapeleka shuleni likiwa na watu 13 -- mwalimu mmoja, wanafunzi 11 na dereva.

Gari hilo aina ya Toyota Hiace, lilianguka kwenye korongo la Sinoni lililojaa maji katika eneo la Dampo mkoani Arusha, saa 12 alfajiri.

Katika ajali hiyo, watoto wanne waliokolewa wakiwa hai baada ya ajali kutokea, huku wengine wakisombwa na maji.

Hadi leo jioni miili ya watoto saba ilikuwa imeopolewa majini kwenye maeneo tofauti.

Pamoja na miili ya watoto hao, upo wa msamaria mwema aliyefariki dunia wakati akisaidia kuwaokoa wanafunzi hao.

Simulizi ya wanafunzi

Glory Daniel (8), mwanafunzi wa darasa la pili akiwa wodini walikolazwa katika Hospitali ya Murieti, amesema matroni wao ambaye ni mwalimu, aliyetajwa kwa jina la Anastazia Emmanuel (27) alimkataza dereva kukatiza, lakini alidharau na kuendelea na safari.

“Kilichosababisha gari letu kusombwa na maji ni anko (dereva) kudharau maneno ya matroni wetu aliyemuonya asipite baada ya kukuta maji yameongezeka tofauti na mwanzo tulivyopita, lakini alimgeukia akacheka na akaendelea na safari,” amesimulia na kuongeza:

“Kabla ya kufika katikati ya maji, gari lilianza kuyumba na kuelea kabla ya kugonga daraja dogo la mbao lililokuwa mbele, tulisikia kishindo kikubwa na vioo vikapasuka, maji yakaanza kuingia ndani kwa kasi.”

Amesema baada ya hapo mwalimu wao alishika gogo lililopo kwenye daraja akamuokoa yeye (Glory) aliyekuwa amekaa naye akamtoa nje.

Anasimulia kuwa dereva alimshika mtoto mwingine na kumtoa nje kwa kushirikiana na watu waliofika kuwasaidia, lakini aliporudi kumchukua mwingine aliona watu wengi wakija, ndipo akamwachia na kukimbia.

“Alikuwa amemshika mdogo wangu anayeitwa Noela baada ya mimi kutaka kumsaidia, lakini aliteleza akarudi kwenye maji akasombwa, mimi nikavutwa na kaka mwingine aliyekuwa juu ya daraja,” amesema mwanafunzi mwingine, Praygod Bernard (10) anayesoma darasa la pili.

Amesema alipojaribu kutoka kupitia dirishani, ili kufikia mti uliokuwa pembeni mwa daraja, aliona wenzake wakitokea dirishani na kusombwa na maji.

“Nilishika mbao ya daraja kupitia dirishani ndipo nikatoka baada ya baba mmoja kunivuta, lakini niliona mtoto wa ‘madam’, mdogo wangu John, Shadrack, Patrician, Morgan, Noela, Abigaeli na mdogo wake na watoto wengine wakitokea dirishani na kusombwa na maji,” amesema.


Kauli ya Zimamoto

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Osward Mwanjejele amesema miili ya watoto hao imeopolewa maeneo tofauti katika korongo hilo.

“Miili minne imepatikana katika mashamba ya eneo linaloitwa Olokii, nje ya mji zaidi ya kilomita 35,” amesema Mwanjejele.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, Awadh Haji amesema wanamshikilia dereva wa gari hilo kwa tuhuma za uzembe.

“Jeshi letu linamshikilia dereva kwa uzembe wa hali ya juu baada ya kuona maji mengi, lakini aliendelea na safari badala ya kusubiri yapungue. Taratibu zikikamilika hatua za kisheria zitafuata dhidi yake,” amesema.

Evance Rafael, aliyeshuhudia tukio hilo amesema gari hilo hupita kila asubuhi kuchukua wanafunzi kuwapeleka shule.

Amesema lilipita asubuhi kufuata wanafunzi, lakini liliporudi maji yalikuwa yamejaa.

“Tulisikia kelele za mama mmoja hapa jirani na kijiwe chetu cha kufyatua matofali, tulipofika eneo hilo tukaona gari la wanafunzi likielea juu ya maji, akasema alimuonya dereva asipite maji ni mengi lakini akawa mbishi,” amesema Rafael.

Amesema walianza kazi ya kuokoa na waliwatoa watu wawili wazima ambao ni mwalimu na dereva, na wanafunzi watatu wakiwa hai, huku mmoja wa kiume akiwa ameshafariki dunia baada ya gari kujaa maji.

Wanafunzi manusura ajali ya gari Arusha wasimulia ilivyotokea

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesema uzembe wa dereva umesababisha gari kusombwa na maji yaliyotokana na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.

Amewataka wananchi kutembelea Hospita ya Muriet kutambua miili ya watoto hao na mtu aliyekuwa anasaidia uokozi.


Hali ilivyokuwa shuleni

Katika shule ya Ghati Memorial, saa tatu asubuhi wazazi walionekana wakimiminika kuulizia hali za watoto wao.

Hata hivyo, walizuiwa getini na mlinzi aliyelifunga, wakaanza kupiga kelele wakieleza wanawataka watoto wao.

Baada ya dakika 25, mwalimu aliyejulikana kwa jina la Mary alitoka shuleni kulielekea geti na daftari la majina ya watoto.

Mzazi mmoja baada ya mwingine walitaja majina ya watoto, ndipo walipokabidhiwa na kuondoka nao.

Akizungumzia tukio hilo, Nembris Lema, mzazi wa mtoto mmojawapo shuleni hapo amesema alipopata taarifa za ajali hiyo aliogopa akaamua kwenda shuleni.

Mwalimu Mary amesema wameruhusu watoto kuchukuliwa na wazazi baada ya kuwasiliana na mwalimu mkuu aliyekuwa eneo la ajali.