Simulizi ya mwanamke aliyepambana na mamba-1

Wazazi wa Marita Malambi, Emma Lolensi na Martin Malambi wakiwa nje ya nyumba yao katika Kijijini cha Dakawa Ukutu, mkoani Morogoro. Marita kwa sasa anapatiwa matibabu Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) baada ya kujeruhiwa na mamba wakati akiteka maji kijijini hapo Februari 17, mwaka huu. Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

Hapo ndipo basi nililoabiri linapoishia na ndipo nilipoelekezwa kwamba nitakutana na wenyeji wangu. Lakini baada ya kuulizia nyumbani kwa mzee Malambi, ndipo ninapogundua kwamba kumbe safari yangu haiishii hapo, nalazimika kutafuta usafiri mwingine na huu ni wa bodaboda kwani wenyeji wananiambia ni kama kilomita tano hivi kutoka hapo.

Ni jioni ya Machi 4 ninawasili katika Kijiji cha Dakawa – Ukutu. Ni baada ya mwendo wa saa nane kutoka Morogoro Mjini. Wanakijiji wanaonekana wapo katika pilikapilika za hapa na pale, ukiwa mpita njia, ni vigumu kujua masahibu yanayowakumba.

Hapo ndipo basi nililoabiri linapoishia na ndipo nilipoelekezwa kwamba nitakutana na wenyeji wangu. Lakini baada ya kuulizia nyumbani kwa mzee Malambi, ndipo ninapogundua kwamba kumbe safari yangu haiishii hapo, nalazimika kutafuta usafiri mwingine na huu ni wa bodaboda kwani wenyeji wananiambia ni kama kilomita tano hivi kutoka hapo.

Baada ya mwendo wa takriban robo saa, nafika kwa wenyeji wangu, mzee Martin Said Malambi na mkewe, Emma Lolensi.

Wazee hawa wanaishi katika kibanda kidogo kilichojengwa kwa udongo wa mfinyanzi, hakijaezekwa vizuri kwa nyasi lakini kina eneo kubwa la wazi.

Wanandoa hawa hawakumbuki siku zao za kuzaliwa lakini kutokana na maelezo wanayonipatia, nabaini kwamba walioana yapata miaka 48 iliyopita na kubahatika kupata watoto wanane, lakini sasa amebaki mmoja pekee ambaye naye hivi karibuni, alinusurika kifo mdomoni mwa mamba. Na huyo ndiye kiini cha safari yangu katika kijiji hicho.

“Maisha kwetu hayana maana. Tumebaki kuomba Mungu amlinde binti yetu huko alipo, lakini hatujui hatima ya maisha yetu ya kesho, kula, kuvaa, kulala yote kwetu yamebaki kuwa mtihani.”

Hivyo ndivyo, Emma ambaye ni mama mzazi wa Marita Malambi (25) aliyeshambuliwa na mamba Februari 17 wakati akiteka maji katika Mto Mgeta unaopita katika kijiji hicho, anavyoanza kusimulia. Katika tukio hilo, Marita ambaye ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yao alipoteza mtoto wake wa kiume na hivi sasa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) akiendelea na matibabu.

“Ulikuwa muda kama huu (saa kumi na moja jioni) nilikwenda kutafuta mboga ng’ambo kufika hapa nikamkuta baba yake kuuliza (Marita alipo) akasema ameenda mtoni na mama yake mdogo, ghafla tukasikia mayowe na watu wakikimbia kuelekea mtoni, nasi tukaenda pia kufika huko namuona mwanangu amelazwa mchangani na mjukuu wangu aliyekuwa amembeba mgongoni hayupo naye,” na hapo machozi yalionekana dhahiri.

Mtoto hakupatikana

Emma anasema baada ya kumuona Marita akiwa katika hali mbaya, jambo la kwanza ilikuwa kumwahisha hospitali na kulipokucha walirudi mtoni kumtafuta mtoto wake, Godfrey David ambaye alikuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi miwili.

“Asubuhi wanaume wakiwa na mishale mikali wamekwenda kumtafuta mtoni, kutwa nzima lakini hawakuona chochote. Tumeishia tu kimya, la kuamua hakuna tena,” baada ya kueleza hayo aliangua kilio na kwa dakika kadhaa alipotulia alisema baada ya tukio hilo, mtoto mkubwa wa Marita alichukuliwa na ndugu wa baba yake kwa matunzo.

Mzee Malambi anasema, “Mjukuu wangu hatujampata baada ya yeye (Marita) kuokolewa, wenzetu wametusaidia mpaka bondeni huko hakuna tulichoona na mpaka sasa tunalia msiba hapa nyumbani hatujazika chochote maana hatujui huenda kaokotwa na mtu huko, kwa kifupi tumechanganyikiwa hatujui cha kufanya.”

Hali ya familia kwa sasa

Familia hiyo inayachukulia masaibu yaliyomfika Marita kama kuongeza jeraha la kidonda kwani Emma anasema alikuwa akiisaidia familia hiyo tangu kaka yake apotee katika mazingira ya kutatanisha Julai mwaka jana alipokwenda shambani katika eneo la ng’ambo ya mto.

“Alipokwenda shamba ng’ambo hakurudi tena, hatujui nini kilimkuta mpaka leo hatujawahi kumuona, akamuacha Marita ndiye aliyekuwa anatusaidia,” hata alipoulizwa kama huenda alikamatwa na mamba akivuka Mto Mgeta, Emma anasema, “Shamba ndiyo shughuli zake tulikuwa tunajua mtoto wa kiume anatafuta hela, wazo hilo nilikuwa sina nilijua yupo sehemu nzuri labda tutaonana naye, lakini mpaka leo hakuna taarifa zake.”

Anasema uchumi wa familia umeyumba, “Hapa nilipo hatuna chochote, hatuna hela wala nini, tumekaa tu mtu atuletee chakula, hatuna usaidizi wowote.”

Mzee Malambi anaongezea alipoishia mkewe akisema kabla ya kushambuliwa, Marita alikuwa kiungo kikubwa katika familia yao kwani licha ya kwamba familia ina mashamba machache, alimudu kufanya kazi za vibarua katika mashamba ya watu ili kuongeza kipato cha familia.

“Tulikuwa tunamtegemea mtoto huyohuyo. Kutulisha alikuwa ni yeye, kuokota kuni, kuchota maji, sasa tumeumwa. Kama unavyoona nyumba hii imechoka inataka kudondoka, alipanga kuikarabati kidogo, muda wote anaangalia familia hapa nyumbani.

“Tunaumia sana hatujui tutafanya nini, kwa sasa majirani wanatusaidia, chukueni chakula mle, tumekosa tunachuma majani tunakula hivyohivyo. Kwa mfano, hapa tangu tumekula kisamvu mchana, ni mpaka kesho tena ndiyo tutajua tunakula nini. Tunachokiomba ni viongozi watusaidie ili maji yawe jirani, tuepukane na vifo vya mamba.”

Mkazi wa kijiji hicho, Mwajuma Said anasema licha ya kutokuwa na mume, binti huyo alimudu kuwatunza wazazi wake na watoto wake wawili licha ya ugumu wa maisha uliokuwa ukiwakabili.

Kama vile alikuwa anajua hatari iliyokuwa mbele yake, Mwajuma anakumbuka jinsi ambavyo Marita alikuwa akiongoza ‘mapambano’ ya kudai huduma ya maji katika mikutano ya kijiji bila mafanikio.

“Nilikuwa namfahamu ni msichana makini na anayejituma sana, si mtu wa makundi na mara nyingi alikuwa akifanya shughuli za vibarua vya mashambani. Hapa kijijini iwapo mtu anatafuta mfanyakazi wa kumlimia au kumfanyia palizi shamba lake, moja kwa moja alitafutwa yeye.

“Sisi hapa kijijini hatuna uamuzi juu ya kadhia hii, hawa mamba leo wameleta msiba kwenye nyumba ya mzee Malambi amebaki yeye na mkewe japokuwa walizaa watoto wanane, tegemeo lao (Marita)anapigania maisha hospitalini.”

Mwanakijiji mwingine Juma Mbuga anamwelezea Marita kuwa ni msichana aliyetegemea kazi za mikono ili kuendesha maisha yake na ya familia yao kijijini hapo.

Anasema Marita hakuwa tegemeo katika familia yao pekee, akibainisha kwamba kile alichokuwa akipata katika kazi zake za vibarua, alikuwa na mtu mwingine aliyekuwa akimsaidia.

“Kuna babu mmoja anaishi pale bondeni, hatujui ataishije sasa kwani Marita alikuwa akipika chakula lazima ampelekee yule mzee kwani anaishi mwenyewe hana mke wala watoto,” anasema Mbuga.

Ilikuwaje siku ambayo Marita, tegemeo la maisha ya familia ya mzee Malambi na jirani yao alivyopambana na mamba?

ITAENDELEA KESHO