Ugonjwa wa kisukari wazidi kuwa tishio

Mwandishi wa Habari kutoka Azam Tv Temaluge Kasuga akichangia damu katika maadhimisho ya ugonjwa wa kisukari duniani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila

Muktasari:

  • Ukubwa wa tatizo la kisukari duniani kote limeendelea kuwa tishio la uhai wa watu mwaka hadi mwaka huku nchini Tanzania takwimu zikionyesha ni watu 9 kati ya 100 wana kisukari.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kati ya watu wazima 100 takribani watu 9 wana ugonjwa wa kisukari, huku kati ya watu wazima watatu mmoja ana shinikizo la damu.

Takwimu hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Lawrence Museru wakati wa maadhimisho ya siku ya kisukari duniani yanayofanyika katika tawi la Mloganzila.

Amesema kufuatia ukubwa wa tatizo hilo, kliniki ya kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ina wagonjwa zaidi ya 6,000 wanaohudhuria kwa mwaka.

“Kama kasi hii ikiendelea hivi, WHO inakadiria kuwa kufikia mwaka 2035 idadi ya wagonjwa wa kisukari duniani itafikia watu milioni 592 na Tanzania watu zaidi ya milioni 3,” amesema Profesa Museru.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kisukari, Elisante Banduka amesema moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari na presha ni mabadiliko ya taratibu na mtindo wa kimaisha ikiwemo ulaji usiofaa.

“Kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, wapo wanaokula mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili, kutokula matunda na mbogamboga kiasi cha kutosha na kula nafaka zilizokobolewa,” amesema.