Wafanyabiashara waiomba Serikali inunue korosho za wakulima

Muktasari:

Zaidi ya tani 13,500 za korosho zimekosa wanunuzi katika minada iliyofanyika hivi karibuni mkoani Mtwara, walikuwa walitarajia kuuza korosho nyingi lakini mnadani wanunuzi waliishia kununua chache

Dar es Salaam. Baadhi ya wanunuzi wa korosho wameshauri Serikali inunue zao hilo ili kuepusha wakulima kupata hasara.

Wamesema hatua hiyo inatokana na wao kushindwa kununua kwa bei ya juu ya zaidi ya Sh3,000 iliyoelekezwa na Rais John Magufuli kwa sababu bei ya wateja wao nje ya nchi haiwaruhusu.

Oktoba 28, baada ya wakulima kugoma kuuza korosho katika minada mitatu mfululizo kwa kile walichoeleza bei kuwa ndogo, Rais Magufuli alishiriki katika mkutano na wadau hao jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine, aliwataka kununua korosho hiyo kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

Katika mkutano huo wa majadiliano kati ya wanunuzi wa korosho na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliungana na wakulima kupinga bei ya wanunuzi ya Sh1,700.

Alisema endapo wafanyabiashara hao hawako tayari kununua korosho hizo wamwambie ili Serikali yake izinunue kwa sababu inajua soko lilipo.

Jana, mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni zinazonunua korosho ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema Serikali haikuwa na haja ya kuagiza bei elekezi na badala yake ilitakiwa kushauriana na wafanyabiashara.

“Msimu uliopita korosho iliuzwa hadi Sh4,000 lakini halikuwa agizo la Serikali, bali soko la nje ndilo lililopanga bei, ndiyo maana mwishoni iliuzwa hadi Sh2,000. Nishauri tu kama Serikali inataka wakulima wasipate hasara inunue hizo korosho itafute soko yenyewe,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wengi hawakuweza kupinga maagizo ya Rais Magufuli wakati alipozungumza nao lakini hali ya soko inawabana na wanashindwa kusimamia walichokubaliana nacho.

Meneja masoko na mauzo wa kampuni moja ya ununuzi wa korosho ambaye naye aliomba kuhifadhiwa jina alisema wanashindwa kununua kutokana na bei kutoendana na soko la wateja wao.

“Soko langu mimi ni Vietnam, huko nimezoea kuuza kwa Dola 2,300 kwa tani moja lakini sasa oda ninazozipata zinataka tani moja kwa Dola 1,400. Hivyo siwezi kununua kwa bei zaidi ya Sh2020 kwa kilo nikifanya hivyo nitapata hasara,” alisema. Alisema anasubiri kama soko litaimarika ndipo anunue akisema kampuni zinazonunua sasa ni zile kubwa ambazo miaka iliyopita zilikuwa zikinunua tani 15,000 hadi 20,000 ambazo sasa zimenunua mamia.

Alisema biashara ya korosho kwa kiasi kikubwa inategemea soko lililopo kwa wakati huo kwani sio bidhaa ambayo unaweza ukainunua na kusubiri ipande bei ndiyo uiuze, “Kadri korosho inavyozidi kukaa inapungua uzito na thamani yake, ni biashara ya muda mfupi”.

Akizungumzia madai ya wanunuzi hao, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alisema wafanyabiashara wengi wameitikia wito wa Serikali kwa kuanza kununua kwa bei elekezi na kuelezea matumaini yake kwamba kiwango kinachonunuliwa kitaongezeka kabla ya kuisha kwa mnada.

“Tusikimbilie kuwaza vibaya hivyo, msimu wa mnada ni miezi mitatu na huu ni mnada wa mwanzo tu, hauwezi kutoa tafsiri ya jumla ya ununuzi wa korosho,” alisema Dk Tizeba alipoulizwa kama anakusudia kumshauri Rais kuhusu Serikali kununua korosho.

Alisema kuna wafanyabiashara ambao bado hawajashiriki mnada na baada ya kufanyika minada kadhaa ndipo watakapopata picha kamili kuhusu mwenendo wa ununuzi wa zao hilo.

“Hili jambo sio la kujengea ajenda sasa kwani lina masilahi ya umma, korosho kwa watu wengine ni maisha,” alisema Dk Tizeba.

Novemba 2, wafanyabiashara kadhaa walijitokeza katika mnada wa kwanza wa korosho mkoani Mtwara baada ya kikao hicho lakini zaidi ya tani 13,500 zilikosa wanunuzi.

Licha ya mnada huo kuhudhuriwa na Waziri Tizeba, kati ya tani 16,000 za korosho zilizotakiwa kuuzwa siku hiyo katika minada miwili iliyofanyika katika mkoa huo ni tani 2,341 sawa na asilimia 14.6 ziliuzwa.

Kwa mujibu wa meneja wa ushirika wa Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), Mohammed Nasoro katika mnada uliofanyika karibuni, tani 7,000 zilipangwa kuuzwa lakini ni 2,141 tu zilizouzwa huku bei ya juu ikiwa ni Sh3,016 na bei ya chini ikiwa ni Sh3,000.

Meneja wa Chama cha Ushirika cha Masasi na Mtwara (Mamcu) Joseph Mnole alisema kati ya tani 9,000 za korosho zilizotarajiwa kuuzwa ni tani 200 tu zilizonunuliwa.