Waitara ataka tathmini ya hasara inayopatikana mradi wa Dart

Muktasari:

Kutokana na utaratibu wa sasa wa ukataji tiketi kwa mabasi yaendayo haraka, Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara ameagiza kufanyika kwa tathmini ili kubaini ni kiasi gani cha mapato Serikali inapoteza.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara ameitaka Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kufanya tathmini ya kujua hasara kiasi gani Serikali inapata kutokana na mfumo wa utoaji tiketi wa sasa katika huduma hiyo.

Waitara ametoa agizo hilo leo Jumatatu Desemba 24, 2018 wakati alipotembelea mradi huo na kuona tiketi za abiria zikichanwa badala ya kuziingiza (scan) katika mashine kama ilivyokuwa awali jambo ambalo amesema linampa hofu huenda kuna upigaji unaweza kufanyika.

"Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu kila mmoja anafahamu tunataka kila senti hapa ilipiwe kodi na kila kiasi kinachokusanywa kifahamike lakini mashine zikiwa hazifanyi kazi kama hivi napata wasiwasi wa upigaji," amesema Waitara.

Katika ziara hiyo, Waitara ametembelea kituo cha mradi huo cha Kivukoni na baadaye kwenda Gerezani amesema yeye binafsi au ofisi yake itafanya tena ziara ndefu ili kubaini changamoto nyingine na ataandaa jukwaa la wadau wote ili kubaini changamoto za pande zote kisha kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayotoa huduma katika mradi huo ya Udart, John Nguya amesema kutokana na mfumo huo kampuni yao inapoteza mapato kwa asilimia tatu mpaka nne ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.