Wakulima waanza kujazwa pesa za korosho

Wakulima wa korosho katika kiji cha Lwelu Mtwara vijijini wakisomba magunia ya zao hilo kwa ajili ya ksafirisha kwenda ghalani.

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema vyama vya ushirika 35 vya Lindi, Mtwara na Ruvuma vimeshakamilisha uhakiki na hivyo wakulima wataanza kuingiziwa malipo yao kuanzia leo.

Mtwara. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema baada ya uhakiki kufanywa katika Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos), vyama 35 kati ya vyama 617 nchi nzima vimekamilisha na vimeanza kuingiziwa fedha kuanzia jana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 16, 2018 mjini Mtwara, Waziri Hasunga amesema baada ya kufanya uhakiki wa wingi wa korosho walibaini kuwapo kwa maghala makubwa 17 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

“Mpaka jana (juzi) kulikuwa na tani 118,192 za korosho zilizokusanywa. Hatua ya kwanza kuimarisha ulinzi, kama mnavyofahamu maofisa wa jeshi wameshakuja. Matarajio ni kuwa na korosho tani 220,000. Bado korosho iko kwa wakulima na vyama vya msingi,” amesema Waziri Hasunga.

“Tunawalipa kama maagizo ya Rais, Sh3,300, kama kuna madai huko mmekopana wamfuate huko huko, sisi tutawalipa moja kwa moja. Mpaka sasa benki wanaingiza fedha kwenye akaunti, japo bado uhakiki unaendelea, mpaka Ijumaa ya wiki ijayo korosho tulizokusanya wawe wamelipwa,” amesema Waziri Hasunga.

Kuhusu magunia 152 ya korosho yaliyokamatwa kutoka nchi ya Msumbiji, Waziri Hasunga amesema hatua ya kwanza waliyochukua ni kuitaifisha, huku pia akionya wakulima na vyama vya ushirika vitakavyoingiza korosho chafu ya msimu uliopita.

“Kuna watu wana korosho chafu na kuna wengine wamekamatwa toka jirani kama mlivyoshuhudia wameshakamatwa. Tutahakikisha korosho toka nje haziingii. Tunaomba wananchi wazalendo watoe taarifa,” amesema.

Mbali na korosho hizo amesema kuna tani 20 za korosho chafu zilizogundulika katika ghala la Olam mjini Mtwara na magunia matano kutoka vyama vya ushirika vya Mnyawi na Mbemba akisema korosho inayolipwa Sh3,300 ni daraja la kwanza tu.