Kivuko cha MV Nyerere chazama Mwanza

Muktasari:

Kivuko cha MV Nyerere kinachofanya safari kati ya Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza kimezama leo Alhamisi Septemba 20, 2018

Dar es Salaam. Kivuko cha MV Nyerere kinachofanya safari kati Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza kimezama leo Alhamisi Septemba 20, 2018.

Akizungumza na MCL Digital Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana amesema kivuko hicho kimezama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara.

“Ni kweli kivuko cha MV Nyerere kimezama kilikuwa kinatoka Bugorora katika Kisiwa cha Ukerewe kuelekea Kisiwa cha Ukara,” amesema.

Kamanda Shana amesema kuwa kivuko hicho kimezama leo mchana  baada ya kupinduka.

“Kiliondoka saa 6 mchana na ilipofika saa nane kamili mchana kilipinduka,” amesema.

Amesema kuwa watu watatu wameokolewa na shughuli ya uokoaji inaendelea ikiongozwa na mkuu wa mkoa huo, John Mongella.

“Mpaka sasa kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mkuu wa mkoa iko eneo la tukio lakini waliookolewa mpaka sasa hivi ni watatu, wengine bado wako humo wakiomba msaada,” amesema.

Amesema bado hawajapata idadi kamili ya waliokuwemo kwenye kivuko hicho.

Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda amekiri kuzama kwa kivuko hicho na yuko njiani kulekea huko na watatoa taarifa baadaye.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, Denis Kwesiga, kivuko hicho kimezama kikiwa mita 50 kutia nanga katika bandari ya Ukara.

Shuhuda huyo amesema kivuko hicho ambacho kinabeba abiria 101 na tani kadhaa za mizigo, hadi sasa zaidi ya watu 20 wameokolewa kutoka kwenye ajali hiyo na kupelekwa kwenye kituo cha afya cha Bwishe.

“Siku ya Alhamisi kivuko hicho huwa kinabeba abiria wengi na mizigo kwa sababu kisiwa cha Ukara huwa ni siku ya gulio hivyo kuna uwezekano wa watu wengi kuzama,” amesema Kwesiga.

Endelea kufuatilia MCL Digital kwa taarifa zaidi