Kombo: Amani, utulivu sababu za watalii kuzuru nchini

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo

Muktasari:

  • Waziri wa habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo amesema miongoni mwa sababu zinazowafanya watalii kufika nchini ni uwepo wa amani na utulivu

Zanzibar. Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo amesema amani na utulivu iliopo Zanzibar ni miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyowafanya wageni wengi kuingia Zanzibar.

Kombo ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa kufuatia uzinduzi wa tamasha kubwa la kitalii linalotarajiwa kuanza Jumatano Oktoba 17, 2018.

Amesema kuna kila sababu kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kudumisha amani iliyopo ili wageni zaidi waendee kutembelea nchini.

Amesema mwaka huu hadi kumalizika kwake wanategemea zaidi ya wageni laki tano watawasili Zanzibar kutoka mataifa tofauti ulimwenguni.

Waziri huyo amesema sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika bajeti kuu ya Serikali kwani imeweza kuchangia asilimia 27 kwenye bajeti kuu ya 2017/18.

Akizungumzia kuhusu tamasha hilo la utalii amesema wanatarajia zaidi ya wageni 150 kuwasili Zanzibar na watapata fursa za kutembelea maeneo mbalimbali ya kitalii Unguja na Pemba.

Kombo ametoa wito kwa taasisi mbali mbali kutumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar ndani na nje ya nchi.