Kubenea amtaka Dk Mpango kumuiga Mgimwa

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea

Muktasari:

Summary: Ametoa kauli hiyo katika mjadala wa bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2018/19

Dodoma. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kufuata nyazo za aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, William Mgimwa kwa maelezo kuwa alikuwa na msimamo na mwenye uamuzi uliolisaidia Taifa.

 

Mgimwa ambaye pia alikuwa mbunge wa Kalenga (CCM) alifariki dunia Januari, 2014  katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic jijini Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.

 

Akizungumza leo Juni 21, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali, Kubenea amesema Mgimwa alikuwa na msimamo kuliko mawaziri wengine katika wizara hiyo.

 

“Hivi Dk Mpango nini unachokifanya hapo, ni kwa nini umeshindwa kumshauri Rais? Kwa nini usimuige Mgimwa ambaye alizuia hata Taifa lisilipe fedha za Escrow,” amesema Kubenea.

 

Amemtaka Dk Mpango kufanya kazi kwa kumshauri vyema Rais masuala ya kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa na wananchi wake.

 

Amesema kwa sasa Taifa halijulikani kama ni la ujamaa au ubepari, huku akidai kuwa mapato ya nchi yanashuka lakini imekuwa ikielezwa kuwa yanaongezeka.