Kupanda na kushuka kwa Rais Robert Mugabe

Harare, Zimbabwe. Vitabu vinavyoelezea kumbukumbu vinaweza kuwa na maandishi mengi kuhusu historia ya Zimbabwe lakini pengine visiwe vimekamilika bila kulitaja jina la Robert Mugabe.

Mugabe aliyetajwa wakati fulani kama mtoto halisi wa Zimbabwe na baadaye kugeuka mwiba kwa raia wake sasa amemaliza enzi ya utawala wake. Alizaliwa Februari 21, 1924 katika kijiji cha Kutuma kilichoko Kusini Rhodesia kabla ya kuwa Zimbabwe.

Alikuwa miongoni mwa vijana wachache waliojitokeza mstari wa mbele kupinga utawala wa Wazungu uliokuwa ukiongozwa na Ian Smith. Ilipofika mwaka 1963 akiwa na lengo kukabiliana na utawala wa Waingereza, Mugabe alianzisha chama cha kisiasa kilichojulikana kwa jina la Zama.

Hata hivyo, chama hicho hakikufanya vizuri katika medani ya kukabiliana na wakoloni na baadaye aliamua kuungana na wapigania uhuru wengine na hivyo kuunda chama cha Zanu-PF.

Mwanasiasa huyo alipata umaarufu mkubwa kwa mara ya kwanza pale alipoongoza vita vya msituni dhidi ya wakoloni walioitawala Zimbabwe, wakati huo ikijulikana kama Rhodesia.

Mugabe alikamatwa na kufungwa jela kwa kipindi cha miaka kumi kufuatia hotuba aliyoitoa mwaka 1964, iliyowaghadhabisha wakoloni ambao waliitaja kuwa ya uchochezi.

Aliachiliwa kutoka jela mwaka wa 1974 na kuingia kwenye siasa za kushinikiza Waingereza kusitisha utawala wake kwa Rhodesia. Baadaye Mugabe alitorokea nchi jirani ya Msumbiji na kurudi Rhodesia mwaka 1979.

Baada ya Zimbabwe kupata Uhuru wake mwaka wa 1980, Mugabe alichuka nafasi ya waziri mkuu, na kuanza kuongoza nchi hiyo chini ya chama tawala cha Zanu PF.

Wengi walimtazama kama mpigania uhuru wa kweli na aliyepigania maslahi ya wanyonge. Lakini sera yake ya kutaka kuwapokonya Wazungu mashamba waliyokuwa wakimiliki nchini Zimbabwe iliibua mgogoro wa kisiasa uliosababisha utawala wake kutikiswa na nchi za magharibi.

Katika miaka ya mwanzo wa uongozi wake, Mugabe alisifika kwa upanuzi wa miundo msingi na huduma za kijamii, zikiwepo hospitali na shule za nchi hiyo. Pia, alishutumiwa kuwa aliwanyanyasa wapinzani wake, wakiongozwa na kiongozi wa upinzani wa wakati huo, Joshua Nkomo.

Tume ya Kanisa Katoliki kuhusu haki na amani ilitoa ripoti iliyodai kwamba zaidi ya watu 20,000 walipoteza maisha chini ya utawala wa Mugabe.

Mugabe alichukua wadhifa wa urais mwaka wa 1987 baada ya nafasi ya waziri mkuu kuondolewa rasmi.

Tangu wakati huo ameshinda uchaguzi mara nyingi licha ya kutajwa na wapinzani wake na waangalizi mbalimbali kama uliojawa na udanganyifu na usiokuwa wa haki na kweli.

Mke wake wa kwanza, Sally Hayfron mzaliwa wa Ghana alifariki dunia mwaka 1992 kutokana na ugonjwa wa figo. Mugabe alimuoa mkewe wa sasa, Grace Mugabe mwaka 1996.