LHRC yataja njia tatu za kupata Katiba Mpya

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba

Muktasari:

Kamati hiyo yaeleza sababu za kukwama kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya

Dar es Salaam. Timu maalumu ya wataalamu iliyoundwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufuatilia mkwamo wa mchakato wa Katiba Mpya imependekeza njia tatu za kupatikana kwa Katiba Mpya.

 

Njia zilizopendekezwa ni Mosi, kuendelea na mchakato kuanzia pale ulipoishia, kwa wananchi kupigia kura Katiba Inayopendekezwa.

 

Pili, kuundwa kwa timu ya wataalamu watakaoandaa rasimu nyingine ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya Ndiyo au Hapana.

 

Tatu, ni kujenga mwafaka wa kitaifa ili makundi yatakayoingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba yawe na dhamira moja ya kuandaa katiba bora kwa maslahi ya Taifa.

 

Akizungumzia mkwamo wa mchakato wa Katiba mpya leo Ijumaa Juni 23, 2018 kiongozi wa timu hiyo, mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk James Jesse amesema mchakako wa Katiba Mpya ulisababishwa na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa.

 

Amesema makundi mbalimbali yalikuwa na malengo tofauti katika katiba, jambo lililosababisha wapinzani kususia mchakato huo na kufanya Bunge liwe la upande mmoja.

 

Amebainisha sababu nyingine kuwa ni uchaguzi wa mwaka 2015 ulisababisha kusimama kwa mchakato huo.

 

Amebainisha kuwa Serikali na vyama vya siasa vilielekeza nguvu zao kwenye uchaguzi huo na kuacha Katiba.

 

"Mwafaka wa kitaifa unaonekana ungekuwa suluhisho na kupatikana kwa Katiba lakini haukuwepo ndiyo maana tunaikumbusha Serikali kuhuisha mchakato huo," amesema.

 

Dk Jesse amebainisha sababu nyingine ya mkwamo huo ni Serikali ya Awamu ya Tano kusisitiza kwamba Katiba Mpya si kipaumbele chake bali maendeleo ya Taifa.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema Katiba Mpya ni moja kati ya ajenda tatu za kituo hicho na wataendelea kuhamasisha kupatikana kwake.

 

Amesema kuna mambo mengi ya muhimu yameondolewa kwenye Katiba Inayopendekezwa kama vile mgawanyo wa madaraka, ukomo wa ubunge na tunu za Taifa.

 

"Tuendelee na mchakato wa katiba Mpya, haijalishi tutaanzia wapi lakini tunataka iwe na mambo muhimu ambayo yaliondolewa kwenye rasimu ya pili ya katiba kama vile tunu za taifa, ukomo wa ubunge, usawa wa kijinsia na mgawanyo wa madaraka," amesema Dk Kijo-Bisimba.