Lukuvi atoa siku 90 halmashauri zimalize migogoro ya ardhi

Muktasari:

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo mbalimbali nchini

Tarime. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi ametoa miezi mitatu kwa halmashauri zote za wilaya, miji, manispaa na majiji kuhakikisha wanamaliza migogoro ya ardhi.

Agizo hilo ameliota leo Septemba 18,2018 mjini Tarime mkoani Mara wakati alipokuwa akiwasikiliza wananchi wenye kero mbalimbali za ardhi na kuwataka wakuu wote wa wilaya kuhakikisha wanasimamia agizo hilo ili kufikia Desemba 30,2018 kusiwe na kero za viwanja.

Waziri Lukuvi amesema Serikali imechoka kusikia migogoro ya ardhi na mipaka ya vijiji inayoendelea nchini wakati masuala hayo yanaweza kutatuliwa na kumalizwa na halmashauri husika.

“Ni aibu kwa watalaamu wa halmashauri hizo kushindwa kutatua kero za wananchi badala yake wanasubiri waziri au kiongozi wa kitaifa kuja kutatua kero hizo wakati miongoni mwa majukumu yao ni kuhakikisha kero hizo zinatatuliwa,” amesema Lukuvi

Lukuvi aliagiza watendaji na watalaamu wa ardhi kwenye halmashauri kufanya ziara katika kila kata, mitaa na vitongoji ili kutafuta kero za ardhi zilizopo.

"Wananchi hawana uwezo wa kuja maofisini kulalamika  na ndiyo maana wanavizia misafara na kuzuia  huku wamebeba mabango juu ya kero  zao sasa nawataka muwafuate huko huko ili muweze kuwahudumia kwa mujibu wa sheria na taratibu" alisema Lukuvi

Mkazi wa Mji wa Tarime, Yohana Mwita alimpongeza waziri huyo kwa uamuzi alioufanya na kwamba hatua hiyo itaondoa migogoro ya ardhi katika jamii ambayo imekuwa chanzo kikuu cha migongano katika jamii.

Amesema kero za ardhi zimekuwa sugu katika maeneo mengi hasa ya vijijini huku wananchi hasa maskini wakiwa hawana la kufanya kutokana na kutokuwa na uelewa wa wapi pa kufikisha kero zao na badala yake wengine wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi.

Naye, Sagini Matiko watendaji hao wakiitumia vizuri hiyo miezi mitatu wanaweza kumaliza migogoro na kero za ardhi maana kwakuwa wananchi wananchi wanashindwa kufanya maendeleo kutokana na migogoro hiyo.