Kimbunga Ialy chapandisha bei ya samaki Dar

Muuza dagaa Soko la Feri, Dar es Salaam, Juma Abdallah akionyesha ndoo ya dagaa ambayo kwa bei ya leo wanauzwa Sh50,000 lakini bahari ikiwa shwari na bidhaa hiyo ikiwa inapatikana kwa wingi huuzwa kuanzia Sh5, 000. Picha na Tuzo Mapunda
Muktasari:
- Wachuuzi wa samaki na dagaa katika soko la Feri wamelalamikia kupaa bei ya bidhaa hiyo, huku wavuvi wakidai samaki wameadimika kutokana na bahari kutokutulia.
Dar es Salaam. Wachuuzi wa samaki wamelalamikia ugumu wa upatikanaji wa bidhaa hiyo katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri jijini hapa, huku wakieleza hata kiasi kidogo kinachopatikana wanauziwa bei ghali.
Bei zilivyo kwa leo Jumanne, Mei 21, 2024 katika soko hilo kapu la dagaa ambalo ujazo wake sawa na ndoo kubwa ya kilo 20 limepanda kutoka Sh5,000 iliyokuwa ikiuzwa siku mbili zilizotangulia hadi Sh60,000, lakini kapu la samaki wadogo imepaa kutoka Sh20,000 hadi Sh80,000.
Wakati wachuuzi wakilalamikia changamoto hiyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jana Jumatatu Mei 20,2024, ilitabiri kimbunga “IALY” kilichotarajiwa kufika katika Pwani ya bahari ya Hindi kinapungua nguvu yake na kitaishia usiku wa kesho Jumatano.
"Kimbunga 'IALY" kinatarajiwa kuisha nguvu yake kabisa usiku wa kuamkia keshokutwa (kesho) Jumatano, Mei 22, 2024. Baada ya kuanza kupungua nguvu na kikielekea kaskazini, mbali na pwani ya Tanzania," ilisema taarifa hiyo.
Mvuvi maarufu katika soko hilo, Bakari Salum 'Chepe' amesema tangu kutangazwa hali mbaya ya hewa upatikanaji wa samaki umekuwa kidogo kwa sababu mitumbwi mingi haiendi baharini.
"Wengi wanaogopa upepo vifaa vichache vinaenda wanatumia gharama kubwa ya mafuta hivyo wanapata hasara biashara wanayofanya hailipi.
"Na wachache wanajitutumua kuingia baharini ni ugumu wa maisha lakini ili familia yake ipate chakula lazima uingie majini na wanapata samaki kidogo hivyo wanauza bei juu kufidia gharama," amesema.
Amesema siku bahari ilikitulia hata wao wanapata riziki nzuri hadi Sh50,000 kwa siku lakini baada ya bahari kuchafuka haendi amesitisha shughuli kwa muda kuhofia usalama wake.
Mchuuzi kutoka Kitunda, Sarafina Nasri amesema amesota kwenye soko hilo tangu asubuhi kusaka dagaa lakini hawapatikani na hata kidogo wanaoletwa kutoka baharini wanauzwa bei juu.
"Unajua tumezoea siku za kawaida dagaa wakipatikana kwa wingi kapu la dagaa tunauziwa Sh5,000 hadi Sh4,000 lakini tangu juzi wamepanda hasa leo kapu tunauziwa Sh50,000 nimeshindwa kununua bajeti yangu haitoshi," amesema.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Oda Komba anayefanya biashara ya samaki wadogo Kimara Korogwe amesema bidhaa hiyo imepanda kiasi cha kuwaongezea ugumu wa kujitafutia kipato.
"Samaki wadogo kapu moja tunauziwa Sh15,000 hadi Sh20,000 lakini kama unavyoona hata ukiuliza hapo Sh80,000 tutaweza kuishi na kusomesha familia kweli? hali ni mbaya," amesema.
Mmoja wa wafanyabiashara wa samaki kwenye soko hilo, Said Ramadhani amesema hali ya upepo imeathiri shughuli zao kiasi cha kuuza dagaa kwa bei juu.
"Asubuhi dagaa na samaki hawa nimenunua kwa bei juu kwa wavuvi kapu la dagaa nimenunua Sh20,000 sasa lazima niuze bei juu kufidia hasara na ukiangalia hapa hakuna sehemu nyingine lazima watakuja kununua tu," amesema.
Mwenyekiti wa soko la Feri, Mbaraka Kilima amesema bidhaa hiyo itaanza kushuka bei baada bahari kuwa shwari na wavuvi wengi kwenda baharini kuvua.
"Shughuli ya uvuvi inaendana na mazingira rafiki ya hali ya hewa, ikichafuka wengi hawaendi kwa sababu wanahatarisha maisha yao," amesema.
Mwananchi Digital imeshuhudia boti zinazofanya shughuli za usafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar zikiendelea kwa kuzingatia ratiba zake huku wasimamizi wakidai hali si mbaya baharini kiasi cha kusitisha usafiri.