Samaki wapungua Ziwa Victoria

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki na boti za kisasa kwa wavuvi kanda ya ziwa iliyofanyika katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza leo Januari 30, 2024. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • TADB yaahidi kusimamia mkopo wa uvuvi usiyo na riba

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2018 na 2022 umebaini samaki kupungua Ziwa Victoria kwa asilimia 35.

Akizungumza leo Jumanne Januari 30, 2024 kwenye hafla ya kukabidhi zana za uvuvi katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, licha ya kutotaja kiasi cha samaki waliokuwamo ziwani kabla ya utafiti huo, amesema sababu ya upungufu huo ni uvuvi haramu.

Mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, atakayekabidhi zana hizo za uvuvi, Makalla amesema kupungua kwa samaki kumesababisha viwanda saba kati ya 15 vilivyokuwapo mkoani Mwanza kufungwa.

“Mkoa wa Mwanza ulikuwa na viwanda 15, lakini vinavyofanya kazi ni vinane,” amesema Makalla.

Amesema mkoa umetoa mikakati na melekezo 11 kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu na kuufanya uwe endelevu, akidokeza kutoa elimu ya vizimba ni miongoni mwa mipango hiyo.

“Mimi kama mwenyekiti wa mikoa ya kanda ya ziwa hatutakuangusha (Rais Samia) tutaweka mikakati ya kuwa na uvuvi endelevu Kanda ya Ziwa,” ameahidi.

Rais Samia atakabidhi boti za kisasa 55 za uvuvi na vizimba 222 kwa wavuvi na vikundi vya uvuvi vya kanda ya ziwa.

Vijana 1,213 kutoka mikoa ya kanda ya ziwa wanatarajiwa kunufaika na mradi wa boti hizo 55, huku wengine 989 wakitarajiwa kunufaika na vizimba 222.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Mkurugenzi Mtendaji, Frank Nyabundege amesema ununuzi wa boti hizo ni sehemu ya mtaji wa Sh57 bilioni uliotolewa na Serikali kwa benki hiyo mwaka 2018.

Amesema kupitia mradi huo, TADB inaamini wavuvi wanaokopeshwa wanakwenda kutajirika kwa shughuli za uvuvi kuzunguka Ziwa Victoria.

“TADB tunasema tunaamini watu wa Kanda ya Ziwa wanaenda kutajirika kwa uvuvi, tunataka kijana ukope, uvue, utajirike," amesema Nyabundege.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe kwa niaba ya watendaji wa wizara hiyo ameahidi kuhakikisha maono ya Rais Samia yanatimia.

"Tutasimamia mradi huu na kuhakikisha wavuvi wanaokopeshwa boti wanalipa mkopo huo ambao hauna riba hata asilimia moja," amesema Profesa Shemdoe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kinajivunia kazi inayofanywa na Rais Samia nchini.

"Tunajivunia kazi unazozifanya, tunatembea kifua mbele kwa jinsi unavyoagiza, unavyozindua, na nakusihi usipunguze kazi," amesema Dk Nchimbi.