Madereva waanza kutii sheria bila shuruti

Muktasari:

Polisi imesema Julai hadi Septemba,2017 ajali za barabarani zilikuwa 1,376 zilizosababisha vifo 655 na majeruhi 1,469.

Dar es Salaam. Madereva wamepongezwa kwa kuanza kubadilika na kutii sheria bila shuruti katika kukabiliana na ajali za barabarani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu amesema hayo akifungua mkutano wa siku mbili wa kupokea maoni kuhusu sheria za barabarani.

Akitaja takwimu amesema Julai hadi Septemba,2016 zilitokea ajali 639 zilizosababisha vifo 923 na majeruhi 2,469.

Amesema Julai hadi Septemba,2017 ajali za barabarani zilikuwa 1,376 zilizosababisha vifo 655 na majeruhi 1,469.

Kamanda Musilimu amesema tatizo la ajali barabarani bado ni kubwa kwa kuwa watu wengi wanafariki na kujeruhiwa.

Hata hivyo, amesema sasa watu wengi wameanza kubadilika na hasa madereva kwa kuwa kuna wakati polisi walilazimika kutumia nguvu nyingi kuwadhibiti.

Amesema jana Jumatatu Desemba 11,2017 nchi nzima kulikuwa na ajali nne ambazo zimesababisha vifo viwili na majeruhi wanne, hivyo ni hatua nzuri.

Ametaka wadau kuhakikisha wanatoa maoni kusaidia kupatikana sheria ambayo haitamkandamiza mwananchi; itakuwa salama; kupunguza ajali za barabarani na inayotekelezeka kwa kupunguza ajali kwa asilimia 50.

Amewataka wananchi waondoe dhana kwamba ajali zinatokana na mapenzi ya Mungu. “Hii si kweli ila matatizo yote ya ajali ni sisi wenyewe tunasababisha kutokana na mwendo kasi na kutotii sheria za barabarani.”