Mahakama kuanza kusikiliza ushahidi anayedaiwa kutapeli kwa jina la Kikwete

Muktasari:

  • Mtuhumiwa anadaiwa kutapeli kwa kutumia jina la Rais mstaafu wa awamu ya nne,  Jakaya Kikwete na mkewe, Salma

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  itaanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya utapeli kwa kutumia jina la Rais mstaafu wa awamu ya nne,  Jakaya Kikwete na mkewe, Salma inayomkabili, Masse Uledi (41).

Mwanamke huyo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kitunda anakabiliwa na mashtaka saba, likiwamo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Facebook.

Hatua hiyo imefikiwa leo katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali.

Licha ya kutumia majina hayo, Masse kupitia akaunti yake ya Facebook anadaiwa kuweka tangazo la vikoba kwa kutumia jina la Jakaya Kikwete Vicoba Saccos, Salma Kikwete Vicoba Saccos na Ridhiwani Kikwete Vicoba Saccos, akionyesha kuwa anatoa mikopo yenye riba nafuu na kisha kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika tangazo hilo, mshtakiwa anadaiwa kuweka namba za simu za mkononi kwa mtu ambaye anataka kupata mkopo apige kupitia namba 0759 142712, 0714 230840 na 0657 076983.

Akimsomea maelezo ya awal, mbele ya Hakimu Mkuu, Thomas Simba, wakili wa Serikali mwandamizi , Partick Mwita, alidai kuwa, Novemba 9, 2017 katika maeneo tofauti jiji la Dar es Salaam, Masse  alijipatia Sh840,000 kutoka kwa Joyce Chitumbi  kama dhamana ya kupata mkopo wa Sh10milioni wakati akijua ni uongo.

Mwita katika shitaka la pili, alidai siku hiyo na eneo hilo Masse alijipatia Sh600,000 kutoka kwa Daniel Cedalia kama dhamana ya kupata mkopo wa Sh2 milioni.

Katika shtaka la tatu, Septemba 28 na Oktoba Mosi 2017, katika maeneo mengine tofauti jiji Dar es Salaam, mshtakiwa anadaiwa kujipatia Sh2.1 milioni  kutoka kwa Lucas Kiula kama dhamana ya kupewa mkopo wa Sh 10 milioni.

Katika shtaka la nne hadi la saba, mshtakiwa anadaiwa kujivaa uhusika usio wake kwa kujitambulisha kupitia ukurasa wake wa facebook kuwa yeye ni Jakaya Kikwete, Salma Kikwete, Reginald Mengi na Getrude Rwakatare kwa lengo la kujipatia fedha kuku akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa huyo anadawa kutenda makosa hayo kati ya Septemba 28, 2017, Oktoba  Mosi na  Novemba 2017 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam.

Mwita alidai mshtakiwa alikamatwa nyumbani kwake akikutwa na simu nane na laini tisa tofauti za simu  ambazo zilikuwa zinatumika kutapeli watu na kisha laini hizo kuzizima.

Masse alipofikishwa polisi alikiri kukutwa na vitu hivyo ikiwamo kujihusisha na utapeli kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, aliposomewa mashtaka yake mahakamani, alikiri taarifa zake binafsi ambazo ni jina lake, kufikishwa polisi na kuhojiwa, kukutwa na simu nane na laini tisa lakini alikana mashtaka yote.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11  itakapoanza kusikilizwa na mshitakiwa yuko nje kwa dhamana.