Maiti iliyofukuliwa Mbeya, yazikwa kinguvu usiku

Muktasari:

Kijana huyo, Baraka Mwafongo, mwenye umri wa miaka 22, alizikwa na Halmashauri ya Mbalizi huku mama yake, Ruth Segeleti akiendelea kushikiliwa na polisi.

Mbeya. Mwili uliofukuliwa Jumamosi na mama aliyekuwa akiamini kuwa mtoto wake angefufuka baada ya siku tatu, umezikwa juzi usiku bila ya ridhaa ya mzazi huyo.

Kijana huyo, Baraka Mwafongo, mwenye umri wa miaka 22, alizikwa na Halmashauri ya Mbalizi huku mama yake, Ruth Segeleti akiendelea kushikiliwa na polisi.

Mama huyo ameendelea kusisitiza maiti ya mtoto wake isizikwe.

Awali Baraka alizikwa Februari 16 katika makaburi ya Mtaa wa Shigamba yaliyopo mji mdogo wa Mbalizi, lakini usiku wa kuamkia Februari 18, mama huyo akisaidiwa na vijana wawili walifukua kaburi na baadaye wakaiweka maiti kwenye pagala ikiwa imevishwa suti ili iombewe na kufufuka.

Kitendo hicho kilizua tafrani kwa wakazi wa mtaa huo na kusababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati kwa kumkamata mama huyo na kuupeleka mwili huo Hospitali ya Rufaa ya Isiki kwa ya kuuhifadhi.

Juzi halmashauri ilifikia uamuzi wa kuuzika mwili huo baada ya wakazi wa Mtaa wa Shigamba walioshiriki mazishi ya awali, kutangaza kutoshiriki kuuzika upya wakisisitiza aliyeufukua auzike upya.

Balozi wa Mtaa wa Shigamba, Shaban Anangisye juzi alisema alitarajia kufanya vikao vya kuwabembeleza wananchi ili wakubali kuuzika mwili huo, lakini walikataa.

Lakini jana, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Shigamba, Yunis Mahenge alisema serikali ililazimika kuuzika mwili huo juzi jioni katika makaburi ya Tanganyika Packers badala ya Mtaa wa Shigamba alikozikwa awali.

Alisema mazishi hayo yalifanyika saa 1:00 jioni yakiongozwa na Sadat Mtwale ambaye ni Katibu Tarafa ya Usongwe, Debora Mrema (mkuu wa kituo cha polisi cha Mbalizi), Kisman Mwangomale (diwani wa Kata ya Nsalala) na ndugu wanne wa marehemu huyo.

Kabla ya mazishi hayo, mchungaji aliyeongoza mazishi ya kwanza yaliyofanyika Mtaa wa Shingamba, Lauden Mwafongo na kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima mkoani Mbeya, Edwini Urio walifika kituo cha polisi kumshauri mwanamke huyo kuachana na imani ya kufufuka kwa mwanawe.

Kiongozi wa kanisa hilo, Urio alisema mwanamke huyo hakuwa muumini wake bali alikuwa akienda kwenye maombi, kauli iliyoungwa mkono na Mchungaji Mwafongo.

Tukio la kufukua kaburi lilitokea Februari 18, Ruth Segeleti alifukua kaburi la mwanaye Baraka kwa imani kuwa atafufuka.

Hata hivyo tukio hilo lilizua taharuki kwa wakazi wa Mji Mdogo wa Mbalizi na baadhi ya wananchi wakachoma nyumba ya mama huyo.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Dhahiri Kidavashari alisema mpaka sasa mwanamke huyo anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.