Wednesday, October 18, 2017

Waandamanaji wachoma moto majengo ya serikali

 

Lome, Togo. Majengo kadhaa ya serikali katika mji wa Sokode ambao ni wa pili kwa ukubwa yamechomwa moto na waandamanaji Jumatatu usiku wakipinga kukamatwa kwa imam na mpinzani mkuu.

Hali hiyo imesababisha Serikali za Canada na Marekani kutoa tahadhari kwa raia wao kuhusu hali ya usalama siku moja kabla ya maandamano makubwa ya siku mbili mfululizo yaliyoitishwa na upinzani kuanzia leo.

Marekani ikikariri amri ya serikali ya kupiga marufuku maandamano imetaja ngomo huo kuwa “hauna kibali” hivyo imewataka raia wake kuchukua hatua za kiusalama popote wanapokuwa. Canada pia imetoa onyo kama hilo ikizingatia hali ilivyochafuka Sokode.

Majengo ya polisi, posta na sehemu ya shirika la mawasiliano ni miongoni mwa yaliyolengwa na waandamanaji waliopambana na maofisa usalama, vyombo vya habari vimeripoti.

Imam Alpha Alhassane kiongozi mashuhuri wa kiroho katika mji huo ni mshauri anafahamika wa chama cha upinzani cha Pan-African National Party kinachoongozwa na Tikpi Atchadam.

Sababu za kukamatwa kwake hazijulikani lakini anahusishwa na mfululizo wa maandamano dhidi ya serikali yanayoratibiwa na upinzani. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya maandamano ambayo yanaripotiwa kusambaa hadi Lome.

Vyama vya upinzani vimeitisha maandamano ya siku mbili dhidi ya serikali nchi nzima kuanzia Jumatano ya Oktoba 18 hadi Alhamisi ya Oktoba 19.

Maandamano ya leo yanamaanisha kwamba wapinzani wamekaidi amri ya serikali ya kupiga marufuku migomo katikati ya siku za kazi.

 

-->