Majonzi yatawala msiba wa mtoto wa Mwakasege

Muktasari:

Viongozi mbalimbali wa serikali na wa vyama vya siasa ni miongoni mwa waliohudhuria misa ya kuuga mwili wa mtoto wa mwalimu Christopher Mwakasege aliyefariki dunia Oktoba 11 jijini Dar es Salaam leo, huku viongozi wa dini wakisifu ushujaa wa mwalimu huyo.

Dar es Salaam. Blanketi la huzuni limewafunika mamia ya waombolezaji wakati wa kuuaga mwili wa mtoto wa Mwalimu wa Neno la Mungu, Mchungaji Christopher Mwakasege, Joshua Mwakasege aliyefariki baada ya kuugua ghafla wakati akiwa kazini.

Joshua aliyekuwa anafanya kazi Benki ya Dunia, Ofisi za Dar es Salaam, alifariki Oktoba 11 katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na dini ni kati ya waombolezaji waliohudhuria ibada ya mwisho ya kuuaga mwili wa Joshua iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT), Mbezi Beach.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowasa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Spika Tulia Anson na Spika Mstaafu Anna Makinda.

Wengine ni wabunge, Nape Nnauye (Mtama) na Mwigulu Nchema (Iramba), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Sefue.

Akihubiri katika ibada ya kuuaga mwili huo, Askofu  wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam,  Jackson Sostenes alisema kifo ni kalenda iliyofichika katika macho na upeo wa mwanadamu kwa sababu hakuna anayejua siku yake.

Amesema hicho ni kipindi kigumu kwa wafiwa na kwamba, wanaendelea kumuomba Mungu azidi kuifariji familia ya Mwakasege.

"Nguvu ya mauti huambatana na uchungu mkali, mauti ndiye adui wa mwisho wa mwanadamu lakini faraja ndiyo dawa yake," alisema Askofu Sostenes na kuongeza;

"Ndugu yetu Joshua ameuvua mwili uharibikao na kuuvaa ule usio haribika. Huzuni ya kifo hiki inaongezeka kwa sababu ni ghafla mno, lakini tuwe na tumaini kwamba ipo siku tutamuona."

Askofu Sostenes alisema binadamu ni mzima sio kwa sababu vipimo vinaonyesha hana ugonjwa, bali ni kwa sababu Mungu ameficha ratiba ya kifo chake.

"Tumezoea kujiunga kwenye kifurushi vya mitandao, ndivyo hivyo katika maisha ya mwanadamu kuna kifurushi cha siku za kuishi ambacho kimeunganishwa na Mungu mwenyewe, hakuna anayejua zimebaki siku ngapi kiishe," amesema.

Amesema kila mmoja amezunguka jeneza la Joshua kuuaga mwili wake lakini hakuna anae jua salio la siku zake za kuishi.

Askofu Sostenes amewapongeza  Mwakasege na mkewe Diana kwa ujasiri walioonyesha ambao licha ya kupokea taarifa za msiba wa mtoto wao, waliendelea kuhubiri kwenye semina iliyokuwa inaendelea jijini Mbeya hadi ilipoisha.

"Mwakasege amejipambanua wazi anaishi anayofundisha, alipita kipindi kigumu lakini hakuiacha kufundisha semina iliyokuwa inaendelea hadi siku ya mwisho ilipofika," amesema.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Masharini na Pwani, Dk Alex Malasusa amesema kanisa hilo linatoa pole kwa familia huku wakimuombea Mwalimu Mwakasege kutokata tamaa kwa kazi ya Mungu anayoifanya.

Askofu wa Kanisa la Efatha, Josephat Mwingira amesema msiba huo ni tukio gumu lakini inawezekana kuupokea.

Kwa upande wake, Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Mbeya, Lugendo amesema wengi walijua Mwakasege angekatisha semina lakini haikuwa hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge, Mbunge wa Hai, Mbowe amesema uwepo wa watu wengi kutoka madhehebu tofauti amemwambia Mwakasege; "Mungu alipenda kutumia tukio hili kukufunua kwa dunia kuhudu huduma yako na kukuwezesha zaidi kutambua kile unachohubiri."

Amesema viongozi wa vyama vya siasa na Serikali wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja ni mpitaji kwenye dunia, hivyo wanapaswa kuishi mahubiri ya Mwalimu Mwakasege.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda aliposimama kutoa Salamu, aliimba wimbo wa Tenzi za Rohoni  usemao ‘Nataka nimjue Yesu na nizidi kumsikia'.

Naibu Spika Dk Tulia amesema Joshua amelala akiwa amemaliza safari yake na hilo ni funzo kwa wanadamu kwa kuwa hakuna anayejua mwisho ni lini.

"Mimi nimejifunza namna ya kulea watoto kupitia msiba huu, wamche Mungu hata wakiwa nasi au peke yao, lakini jingine ni kuishi yale tunayozungumza. Kifo hiki ni funzo kwetu," amesisitiza.

Spika mstaafu, Anna Makinda amesema alimfahamu Mwalimu Mwakasege wakiwa kwenye semina nchini Uingereza.

“Kitabu kile kilikuwa kinasema unapojenga nyumba usijenge vyumba vitatu, jenga nyumba ambayo inamfanya mtoto awe na amani nyumbani kwao hata wageni wanapokuja. Najifunza mengi kwa Mwakasege, pole sana kwa msiba," amesisitiza.