Kutoka kuwa zao la chakula, Muhogo sasa wapaa kibiashara

Muktasari:

Katika nchi nyingine mbali ya kuwa kinga ya njaa, muhogo pia ni zao la biashara na hutumika kutengeneza chakula cha mifugo na malighafi kwa viwanda.

Kwa muda mrefu zao la muhogo limekuwa likilimwa nchini kama zao la chakula na jamii nyingi. Muhogo pia hulimwa na nchi zaidi ya 90 duniani.

Katika nchi nyingine mbali ya kuwa kinga ya njaa, muhogo pia ni zao la biashara na hutumika kutengeneza chakula cha mifugo na malighafi kwa viwanda.

Kwa Tanzania uzalishaji wa muhogo upo chini ya kiwango cha kimataifa, ambapo wakulima hupata kati ya tani tano hadi saba kwa hekta badala ya tani 10.

Habari njema kwa wakulima

Hivi karibuni, zao la muhogo limeibuka kuwa zao muhimu la biashara na huenda wakulima wengi wakatajirika. Hiyo ni kutokana na taarifa za kuwapo kwa soko la nchi ya China na mipango ya Serikali kufungua viwanda vya kuchakata.

Akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alisema Serikali ina mpango wa kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na soko la muhogo la China.

Alisema ili kufikia hatua hiyo, Mei,2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China.

Amesema kufuatia hatua hiyo, Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo katika jimbo la Shandong, huku akisema kwa sasa nchi hiyo inahitaji tani150,000 kwa mwaka.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage anasema licha ya utata wa soko la China, tayari mwanga umeanza kuonekana. “Sisi ni miongoni mwa taasisi za Serikali tuliolifuatilia soko la muhogo la China kwa muda mrefu. Tatizo lao wana masharti magumu, lakini kuna ujanja tumeshaufanya na tumeshafanikiwa,” anasema Waziri Mwijage.

Anaongeza: “Shida ya Wachina wanataka wadhibiti zao tangu likiwa shambani. Wajue muhogo umelimwa wapi, umeanikwa wapi unauzwaje. Lakini tayari kuna mwanga umeonekana kwani kuna kontena moja limeshatumwa kwa majaribio na limekubaliwa. Baada ya hapo tutaanza kupeleka.”

Anasema tayari kuna itifaki ya afya iliyosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na China na Tanzania na kwamba kuna mkataba unaotakiwa kusainiwa na Wizara ya kilimo siku za usoni.

Wasemacho wakulima

Idd Omari anayelima zao hilo katika mikoa ya Tanga, Mtwara na Lindi anasema awali zao hilo walilitegemea kwa chakula lakini sasa liko kibiashara zaidi.

“Mimi niliamua kuzalisha muhogo kibiashara baada ya kupewa mafunzo ya taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation mkoani Mtwara yakihusisha pia Wakala wa kudhibiti mbegu Tanzania (Tosci),” anasema na kuongeza:

“Awali muhogo ulizalishwa kwa ajili ya chakula hasa kwenye mikoa yenye ukame na upungufu wa chakula. Wakulima wengi walitumia mbegu za kienyeji zisizo na sifa huku soko lenyewe likiwa halieleweki.’’

Anasema kuwa wakati huo wakulima waliuza muhogo shambani kwa matenga ya Sh25,000 hadi 40,000. Baadaye wakawa wanauza viroba vya kilo 50 na kilo 100 kwa Sh40,000 hadi 50,000.

Philipo Ntongolo ni mkulima wa muhogo mwenye shamba la ekari 60 katika kijiji cha Bungu wilayani Kibiti. Anasema endapo mikakati ya uhakika itafikiwa kwa soko la China, wana uhakika wa kupata muhogo wa kutosha kwani wakulima wamehamasika vya kutosha.

“Tumetembelea wakulima mbalimbali nchini, tumegundua wengi wamehamasika kulima muhogo. Kwa hiyo tuna uhakika wa kulisha soko la China. Isistoshe kwa sasa kuna mbegu ambayo shina moja linatoa kilo 45 kwa hiyo tunawahamasisha kutumia mbegu hiyo inayoitwa Kiroba,” anasema.

Hofu kwa wakulima na utata wa soko la China

Hata hivyo, baadhi ya wakulima hawajapata mwanga wa soko hilo, badala yake wamejikita kwenye soko la ndani linaloonekana pia kushika kasi.

Akizungumzia fursa ya soko la China, Omari anasema wamefanya uchunguzi na wakulima wenzake wakaona bado halijakaa sawa.

“Ni kweli kwamba zao la muhogo halijawekewa mfumo mzuri wa masoko kama vile mazao ya pamba, korosho na kahawa, lakini tumechunguza hilo soko la China, bado halijakaa vizuri. Ni bora tuendelee kuuza hapa hapa nchini,” anasema.

Omari ni miongoni mwa wakulima walioungana na kuunda kamati maalum ya kufuatilia masoko ya muhogo ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya wakulima wa muhogo, Philipo Ntongolo anasema utafiti walioufanya tangu Juni 7 mwaka huu umeonyesha bado soko la China halijakaa sawa hivyo wanalenga kuanza na masoko ya ndani kabla ya kulifikia.

“Kamati ilitaka kujua muhogo uliopelekwa China, ulikwendaje? Je, taarifa kuhusu nchi hiyo kuhitaji zaidi ya tani 100,000 na ni utaratibu gani unafuatwa kufikia soko hilo,” anasema.

Hata hivyo, anasema wakati wanatafakari soko hilo la China, wamebaini kuwa nchi ya Rwanda imekuwa ikinunua muhogo kutoka Mkoa wa Kigoma kwa Sh800 kwa kilo na kusafirisha katika nchi za Ubelgiji na Urusi.

Ushirika wa wakulima wa muhogo

Kutokana na unafuu wa soko la ndani, Ntongolo anasema wameamua kuunda ushirika wao, ili kukusanya mazao kwa wakulima na kutafuta masoko.

“Endapo ushirika utafanikiwa, wakulima tunaweza kujenga kiwanda chetu binafsi ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchakata makopa na wanga. Tunaweza kujenga viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo, soda, juisi na chakula cha samaki wa kufugwa,” anasema.

Jinsi ya kulima muhogo

Mambo ya kuzingatia katika kilimo cha muhogo ni pamoja na hali nzuri ya hewa na maeneo yenye udongo mzuri usiotuamisha maji. Mvua inayotakiwa ni ya wastani ambayo si kidogo sana na wala si nyingi sana.

Eneo linalolimwa muhogo linapaswa kuangaliwa historia yake ili kuelewa kama kuna magugu hatari na wadudu au magonjwa kwenye eneo hilo, ili kubuni mbinu za kuyazuia au kuyaangamiza mapema.

Epuka kupanda muhogo kwenye eneo lenye mwamba chini kwani hii husababisha mizizi kutonenepa na kuwa na mavuno hafifu. Shamba la muhogo linatakiwa kupandwa mwanzoni mwa msimu wa mvua ili kupata mavuno mengi (Oktoba hadi Machi na Aprili).

Mbegu

Kipando kinatakiwa kiwe na urefu wa sentimeta 25-30 ili upate ustawi mzuri. Urefu wa kipando hutegemea na umbali kati ya jicho na jicho na idadi ya macho. Inashauriwa kipando kiwe na macho kati ya 5 hadi 7, kwani ndicho chanzo cha mizizi na majani.

Pingili zinatakiwa kukomaa vizuri kwani huchangia kwenye ubora na wingi wa mazao yatakayovunwa.

Mbegu haipaswi kuwa na dalili za mhatari, hivyo mkulima achague mimea isiyo na wadudu au magonjwa na zipandwe mapema baada ya kukatwa.