‘Msaragambo’ kutumika kumaliza uhaba wa matundu ya vyoo

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chanika wilayani humo mkoani Tanga. Picha na Maktaba


Halmashauri ya Handeni iliyopo Mkoani Tanga imeamua kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi lengo likiwa ni kutaka kumaliza tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo hasa katika shule za msingi linalozikabili shule nyingi za msingi.

Inaelezwa kuwa idadi inayohitajika ni matundu 3,308 na mpaka sasa wanayo matundu 948 pekee katika shule zote za msingi wilayani humo.

Akizungumza hivi karibuni wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe anasema matundu ya vyoo yanayohitajika hadi sasa ni 2,360.

Uhaba huo ndiyo uliomuibua mkuu huyo wa wilaya ambaye sasa ameagiza kila Jumamosi iwe ni siku ya wakazi wote wilayani humo kufanya kazi kwa kujitolea maarufu ‘Msaragambo’ ili kuanza utekelezaji wa ujenzi wa vyoo vya shule.

Naye Ofisa Elimu Wa Wilaya ya Handeni Charles Hizza amekiri kuwepo kwa upungufu huo wa matundu ya vyoo katika shule za msingi zipatazo 118 zilizopo Handeni pia mbali ya upungufu wa matundu ya vyoo wanakabiliwa na uhaba wa uhaba wa nyumba za waalimu.

William Mwakufwe ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, naye anakiri halmashauri yake kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo hasa upande wa shule za msingi na tayari wamejiwekea mikakati endelevu ya kuchimba na kujenga vyoo kwa idadi maalum kila mwaka. Anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo, uongozi wilayani humo umewataka wananchi kufanya kazi za kujitolea kila Jumamosi na watapangiwa maeneo ya kuchimba matundu ya vyoo.

Mkurugenzi huyo amekwenda mbali zaidi kwa kusema halmashauri yake kwa kushirikiana na wadau watajitahidi kuhakikisha matundu hayo ya vyoo yanachimbwa na kwa mwaka huu wamejiwekea malengo ya kuchimba matundu 150.

“Lengo la kuchimba idadi hiyo ya matundu ya vyoo ni kupunguza tatizo hili kwa wanafunzi wetu hasa wanaosoma shule za msingi,” anasema Makufwe.

Hali ikoje upande wa shule za sekondari

Makufwe anasema hali ya vyoo kwa upande wa shule za sekondari ni tofauti na ile iliyoko katika shule za msingi.

Anasema licha ya kuwapo kwa changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule nyingi za msingi, pia hali ni mbaya zaidi kwa wakazi wa Handeni hali iliyosababisha halmashauri yake kuwahimiza wananchi wajenge vyoo na kuona umuhimu wake.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekuwa akisisitiza kupitia kauli ya ‘Nyumba ni Choo’ akiwa na lengo la kuwataka wananchi waanze kuona umuhimu wa kujenga vyoo bora kuanzia kwenye familia na hatimaye katika taasisi na shule.

“Hivi sasa halmashauri inatekeleza mpango wa kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na choo bora cha kisasa na safi kwa kila kaya kwa sababu kwenda kujisaidia vichakani au kutumia matundu ambayo hayana usafi wa kutosha siyo afya kwa maisha ya binaadamu wa karne ya sasa,” anasema Makufwe. Anasema halmashauri ya Handeni inalazimika kutoa elimu ya umuhimu wa wa kuwa na matundu ya vyoo kwa kila kaya huku wakishirikiana na wadau mbalimbali na akasisitiza ni wajibu wa kila mwananchi kuchimba matundu ya vyoo kwani ni muhimu kwa afya zao.

“Hatuwezi kwenda kuwajengea vyoo wananchi, hiyo fedha hakuna, hivyo jambo kubwa tunalolifanya ni kutoa hamasa kwao wajenge utaratibu wa kuwa na vyoo bora safi na salama kwa afya zao, pia tunawashukuru wadau wetu Word Vision, nao wamekuwa na msaada mkubwa katika kampeni hii ya ujenzi wa vyoo bora hapa Handeni,” anasema. “Huu ni mpango madhubuti na endelevu wa kupambana na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo na nitahakikisha tunapiga hatua kubwa katika kampeni hii.”