Kauli ya Obama yashuka na kiu ya Katiba imara

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Obama, siasa za kuwatia watu hofu, kutoridhika na kuwa na misimamo mikali, zilianza kuwavutia watu na kwamba kwa sasa siasa za aina hiyo zinashika kasi barani Afrika na kwamba inaonekana ni kama dunia inaelekea kwenye siasa za kukaripiana.

Ni mjadala mpya kuhusu kauli ya Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama kuwa viongozi wengi duniani wana tawala kwa ubabe. Mengi yanasemwa na kubwa linalochomoza ni kiu ya Katiba imara.

Kwa mujibu wa Obama, siasa za kuwatia watu hofu, kutoridhika na kuwa na misimamo mikali, zilianza kuwavutia watu na kwamba kwa sasa siasa za aina hiyo zinashika kasi barani Afrika na kwamba inaonekana ni kama dunia inaelekea kwenye siasa za kukaripiana.

Anaongeza kwamba ni lazima kuwa macho dhidi ya watu wanaojaribu kujitukuza kwa kuwashusha hadhi wengine.

Mapema wiki hii Rais huyo mstaafu wa Marekani alipokuwa akihutubia katika mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela nchini Afrika Kusini ambao huandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa zamani, Obama alisema kuwa baadhi ya viongozi wanatawala kwa ubabe, huku wakiikandamiza demokrasia na kuuweka ulimwengu njiapanda.

Kutokana na kauli hiyo ndipo ukaja mjadala wenye sura ya kuhitaji Katiba imara. Wadau mbalimbali wanasema Obama amezungumza uhalisia wa kinachotokea sasa katika nchi za Afrika, na hata Tanzania na kutaja mambo kadhaa ambayo yanaweza kuiondoa nchi katika hali hiyo.

Wakati Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatuma Karume akisema kuwa njia pekee ya kubadili hali hiyo ni kwa wananchi wenyewe kupaza sauti, wadau wengine mbalimbali wanasema suluhisho la hali hiyo ni kuwa na Katiba imara.

Katiba itatuondoa tulipo

Wakili wa kujitegeme Peter Mshikilwa anasema ili Tanzania kuondokana na hayo ni lazima kutengeneza taasisi imara ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na Katiba itakayoelezea taasisi hizo na majukumu yake.

“Katiba ya sasa ina mapengo mengi, Rais anabaki peke yake amepewa mamlaka makubwa; tunatakiwa tutoke hapo. Mfano wenzetu Kenya sasa wana Katiba inayozingatia hali halisi ya nchi yao,” anasisitiza.

“Kwetu ni tofauti, kila kukicha katika chaguzi zetu kuna malalamiko hii inatokana na kutokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi,” anaongeza wakili Mshikilwa.

Mshikilwa anasema kuwa hayo yote yanasababishwa na mfumo uliopo unaoruhusu wasimamizi wa uchaguzi kuwa wakurugenzi wa halmashauri, jambo ambalo anadai si sahihi kwa kuwa mfumo huo hauwezi kutoa haki sawa kwa wagombea.

Wakili huyo anasema kuwa licha ya jitihada zikiwamo za mapambano dhidi ya rushwa zinazofanywa na Rais John Magufuli, ikiwa hakuna msingi bora ni kazi bure.

“Hatukatai kwamba kuna jitihada zinazofanywa lakini hakuna mfumo madhubuti na matokeo yake Rais sasa anafanya kazi mwenyewe; ukienda hospitali mambo ni yaleyale, ukienda mahakamani halikadhalika, kwa kuwa tu watu wanafanya kazi kwa kusukumwa. Akishaondoka anayewasukuma mambo yanaendelea kama kawaida, kinachopaswa ni kutengeneza mfumo wa kisheria na kuwa na Katiba bora kwani Katiba ni maisha,” anaisitiza Mshikilwa.

Mbali na maoni ya wakili huyo, Rais wa TLS, Fatuma Karume anasema kwa hali ilipofika wananchi wanatakiwa kupaza sauti.

“Wasikate tamaa kwa sababu tu mikutano ya siasa na maandamano yamepigwa marufuku, watumie njia mbadala kupasa sauti zao kwa kutumia mitandao ya kijamii,” anasisitiza Fatuma.

Fatuma anasema kwa sasa viongozi wamehakikisha wanawafunga mdomo wananchi, lakini hilo lisiwatishe na kuendelea kukaa kimya, badala yake wapaze sauti zao ili kujikwamua na kadhia hiyo.

“Haki ya kidemokrasia ipo kikatiba, ingawa kuna viongozi wanaofanya makusudi kuiminya, lakini hilo lisiwatishe.

“Ni wananchi wenyewe wanaweza kubadili hali hii, usidharau kura yako ipo siku itafika mahali itakuwa na maana kubwa na kubadili hali ilivyo sasa; wananchi wakiamua wanaweza it’s a matter of time (ni suala la muda tu),” anaongeza.

Haja ya kujitafakari

Katika mtazamo tofauti, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui anasema kwa sasa ipo haja ya kujitafakari tulipo na tuendapo badala ya kuendelea kujidanganya kila kukicha kwamba Tanzania inafuata misingi ya demokrasia.

“Demokrasia ilikuwapo kwa muda mrefu lakini sasa hali ni tofauti kwa kipindi cha miaka miwili tumeshuhudia mabadiliko makubwa, demokrasia inakanyagwa, mikutano inazuiwa hicho ni kielelezo kwamba hatuna demokrasia ya kweli,” anasisitiza Mazrui ambaye anamuunga mkono Katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mazrui anasema imefika wakati kwa viongozi wa nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kuyazingatia yote aliyosema Obama na kuyatekeleza kwa vitendo.

“Nimeisikiliza hotuba ile zaidi ya mara tatu, alichosema ni kweli kabisa, utadhani anatusema sisi Tanzania; ni ukweli mtupu tusipuuze mawazo yake tuyafanyie kazi,” anasisitiza naibu katibu mkuu huyo.

Mwanasiasa mwingine ambaye hayuko mbali na mawazo hayo, ni Ngemela Lubinga, katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM anayehusika na uhusiano wa kimataifa ambaye anawataka wananchi kupigania haki yao.

“Wananchi wenyewe waongee na kupigania haki yao, lakini wasitumiwe na watu, kikundi au taasisi yoyote,” anashauri Lubinga.

“Jambo jingine analoona Lubinga ni kwa viongozi wenyewe kuheshimu Katiba na kusimamia mambo ya msingi kama suala la uchaguzi ili kutoa haki ya kuchagua au kuchaguliwa kwa lengo la kuwa na wawakilishi bungeni.”

Mjadala huo haukumuacha mbali, Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DSM), Dk Benson Bana anayetaka kila kiongozi atafakari ujumbe huo wa Obama.

Lakini, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Shoo Innocent anasema njia pekee ya kujikwamua ni kuupa nguvu Umoja wa Afrika, akisema kwa sasa hauna meno jambo linalochangia nchi wanachama kushindwa kuuheshimu.

“Hiki ndiyo chombo cha juu kwa Waafrika kukutana na kutatua matatizo yetu, lakini ilivyo sasa imebaki kuwa tu sehemu ya kufanya mikutano na washiriki kufanya shopping (ununuzi) pekee. Hakiko strong (imara),” anasema.

“Ni lazima bajeti ya chombo hiki iimarishwe kwa wanachama wake kuchangia asilimia kadhaa.”

Mhadhiri huyo wa masuala ya diplomasia anaongeza kuwa njia nyingine ni kwa nchi za Afrika kuwa na jeshi imara ambalo litatoa msaada pindi unapohitajika badala ya kusubiri kuomba msaada kwa nchi za Magharibi.

“Jambo jingine ni viongozi wenyewe waheshimu demokrasia, kusimamia utawala bora pamoja na kusimamia ipasavyo katiba za nchi zao.”

Pia, anashauri kupunguza vikwazo na vipingamizi katika masuala mbalimbali kama biashara na mwingiliano katika suala la forodha.

“Lakini, hayo yote hayawezi kufanikiwa bila kuwa na elimu bora ambayo itaenda sambamba na maisha ya sasa,” anasisitiza.

“Pia, siasa zetu zisiwe za mgawanyo na kikabila, tuache mila za kizamani ambazo zimepitwa na wakati ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi sawa wanawake katika masuala mbalimbali ya nchi.”

Kauli iwe mwongozo

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema kauli ya Obama iwe ndiyo njia ya viongozi wengine hasa Tanzania kuzingatia na kusimamia demokrasia na kuacha ubabe.

“Wayachukulie kwa uzito maneno ya Obama na kuyafanyia kazi, haiwezekani leo kiongozi Afrika anajitangaza kuwa ameshinda kwa asilimia 90 kana kwamba hakukuwa na ushindani,” anaongeza daktari huyo wa binadamu.

“Hii inawezekana tu kwa viongozi ambao hawatoi ushindani sawa na haya tumeyashuhudia hata hapa kwetu.”

Mashinji anaungwa mkono na John Mrema, mkurugenzi wa itifaki na mawasiliano ya mambo ya nje wa Chadema, anayewataka viongozi wa Afrika wafikirie kama watapenda kutendewa haya wanayoyatenda sasa siku watakapokuwa wastaafu.

Mrema anasema hatari anayoiona ni kwa watu kuchoka utawala wa aina hiyo na kuchukua hatua zinazoweza kuigharimu.

“Ukiwatendea ubabe na kuwafunga midomo, watu wanatafuta njia mbadala ya kupumua. Chondechonde wasiwalazimishe watu kufika huko kwani si pazuri,” anasisitiza.