Kilimo cha mkonge kiimarishwe kuwanufaisha wananchi Tanga

Muktasari:

  • Licha ya Serikali kuelekeza nguvu kuimarisha mazao matano ya biashara, wakulima wa mkonge mkoani Tanga wanaomba yawepo mazingira bora ili kuongeza uzalishaji wa zao hili kwa ajili ya viwanda vilivyopo mkoani humo.

Wakati baadhi ya wananchi wakiwa hawaielewi vizuri dhana ya uchumi wa viwanda, hali ni tofauti mkoani Tanga hasa kwa wakulima wa mkonge ambao wanapendekeza mazingira yaboreshwe zaidi kuwahakikishia soko la mavuno yao.

Tanga ni maarufu kwa kilimo cha katani kwa muda mrefu. Kutokana na uzalishaji wa uhakika wa zao hilo, Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mkonge duniani ikishika namba mbili, nyuma ya Brazili inayoongoza.

Wananchi wengi mkoani humo wanalitegemea zao hilo kukidhi mahitaji yao.

Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Makuyuni, Habiba Mbelwa anasema pamoja na changamoto zilizopo, bado wananchi wanaweza kuendesha maisha kupitia kilimo cha mkonge hivyo kutekeleza dhana ya uchumi wa viwanda kwa vitendo na kuitaka Serikali kuweka mazingira mazuri zaidi kukisimamia kilimo hicho. “Tunapata mafanikio. Na tunapozungumzia uchumi wa viwanda, wakulima wa mkonge Mwelya tunavyo, tunachotaka ni Serikali kukitilia mkazo na kutuwezesha kupata mtaji na kuondokana na ucheleweshaji wa malipo yanayofanywa nje ya wakati,” amesema Habiba.

Mkonge

Historia inaonyesha zao la mkonge liliingizwa nchini mwaka 1892 na Dk Richard Hindorff, mtafiti wa mimea na udongo. Mjerumani huyo alibeba miche 1,000 kutoka pwani ya Mexico kwenye jimbo la Yuctan ambalo ambalo ndilo asili ya jina katani na kuisafirisha mpaka nchini.

Kati ya miche aliyobeba mtaalamu huyo, ni 62 tu iliyofika Tanganyika na kupandwa Kikokwe katika Wilaya ya Pangani. Mpaka mwanzo mwa miaka ya 1960, mkonge ulikuwa umesambaa maeneo mengi na Tanganyika ikawa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge ikifatiwa na Brazil na Mexico. Ilikuwa inauza tani 230,000 nje ya nchi kwa mwaka.

Kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza miaka ya 1970 uzalishaji ulipungua kutoka tani 230,000 hadi tani 19,700 mwaka 1997.

Juhudi za kufufua kilimo cha mkonge zilipandisha uzalishaji mpaka tani 40,000 mwaka 2015 kutokana na ongezeko la mahitaji ya mkonge na bidhaa zake na kupanda kwa bei hasa katika soko la dunia.

Kuanzia mwakani, wadau wa zao hilo wanakusudia kuongeza uzalishaji kutoka tani 34,589 zilizovunwa mwaka huu mpaka tani 100,000.

Mataifa mengi hutumia mkonge kutengeneza bidhaa tofauti kama vile kamba, nyuzi, karatasi, bodi za mchezo wa vishare, mataulo, machujio, mazuria, ngozi ya nyaya na vitambaa vya mkononi.

Soko kuu la mkonge wa Tanzania lipo katika mataifa ya China, Saudi Arabia , India, Uhispania, Ujerumani, Uingereza, Kenya, Uganda na Nigeria.

Wakulima

Wakulima wadogo wa mkonge mkoani Tanga wananufaika na viwanda vilivyopo kikiwamo cha Katani.

Kampuni hiyo ilianzisha utaratibu wa kuwashirikisha wakulima wadogo ili kukidhi mahitaji ya malighafi kwa kuanzisha mpango wa wakulima wadogo (Siso). Utekelezaji wa mpango huo umeonyesha kuimarisha kipato cha wakulima waliochangamkia fursa.

Mmoja wa wakulima hao wa wilayani Korogwe, Mohamed Mgaya anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mazao mengine kama mahindi hayakuwa na mavuno mazuri kutosheleza mahitaji ya mkulima kila msimu lakini mkonge umesaidia kuwainua kimaisha.

“Wakati tunaanza hali ilikuwa mbaya lakini baada ya kupambana sasa hivi tunafaidi matunda yake kwani tumejenga nyumba, tuna magari ya usafiri na bajaji za biashara. Kabla ya hapo, nikiwa mstaafu serikalini, sikuwa hata na baiskeli,” anasema Mgaya.

Hivi karibuni kulikuwa na ucheleweshaji wa malipo ya wakulima walio kwenye mpango wa Siso wa kampuni ya Katani Limited jambo lililomshawishi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela kuingilia kati. Hata hivyo, Mgaya anaamini suluhu ya jambo hilo itapatikana muda si mrefu na wao wataendelea na uzalishaji kama kawaida.

Mkulima mwingine, Ernest Mhina anayefanya shughuli hizo tangu mwaka 2010 anasema mkonge umemuwezesha kununua mashamba ya mahindi na kuendesha maisha yake bila tatizo.

“Nimesomesha wanangu na naendesha maisha kutokana na mkonge. Serikali iongeze hamasa ya kuboresha kilimo hiki ambacho kinatufaa kama ilivyo kwa korosho mikoa ya kusini au pamba ama madini kanda ya ziwa,” anasema Mhina.

Kama walivyo wengine wanaofanya mambo ya msingi kwa kipato wanachokipata, Mariam Mussa anasema ameweza kuitunza familia yake licha ya mumewe kufariki siku nyingi. “Nimeweza kumsomesha mwanangu hadi Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro. Anaelekea kumaliza sasa. Nimejenga na kuweka umeme kwa kilimo cha mkonge,” anasema Mariamu.

Kiwanda cha Katani Limited

Takwimu zinaonyesha kuanzia mwaka 1999 mpaka mwaka jana juhudi mbalimbali zilizowashirikisha wakulima wadogo mkoani tanga zimesaidia kuongeza kipato chao.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Juma Shamte anasema mpango Siso ulianza kuwalipa wakulima hao kuanzia mwaka 2005 uvunaji ulipoanza katika mashamba yao ambayo walipewa na kampuni hiyo.

Upandaji ulianza katika eneo la hekta 30 uliozishirikisha kaya 54 katika Shamba la Mwelya na hadi mwaka 2017 upandaji umeongezeka mpaka hekta 8,268 ukihusisha kaya 1,267 za wakulima katika mashamba ya Magoma, Magunga, Hale, Ngombezi na Mwelya yenye jumla ya hekta 20,000.

“Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka jana, kiwanda kimetumia jumla ya Sh20 bilioni kuwalipa wakulima wadogo 2,100 waliopo chini ya mpango wa Siso,” anasema Shamte.

Wakati wakulima wameanza kushirikishwa, anasema mwaka 2005 uzalishaji wa singa ulikuwa tani 849 ambazo zimeongezeka hadi tani 4,587 mwaka 2017 na mapato yao kupanda kutoka Sh139 milioni hadi Sh3.743 bilioni 3.743 ndani ya kipindi hicho.

Kilichofanyika ni kuwawezesha wakulima kwa mtaji wa kuandaa, kupanda na kuhudumia mashamba yao. Mpaka mwaka jana, Katani Limited imetoa mikopo ya Sh8 bilioni huku yenyewe ikiimarisha mashine za kuchakata mkonge.

Kwa muda huo, kiwanda hicho kimejenga korona nne na kukarabati tatu kati ya 10 zilizopo katika mashamba hayo ili kuwahudumia wakulima.

“Kampuni sasa hivi ipo kwenye uwekezaji wa muda mrefu na inaendesha korona zilizopo kama vituo vya huduma za ugani, masoko, fedha, pembejeo, uhandisi, usindikaji na utafiti kuhakikisha wakulima wanapata mahitaji yote ya kuendesha shughuli zao,” anasema

Lakini kutokana na mgogoro uliotokana na kucheleweshwa kwa malipo ya wakulima wadogo, korona nane za kampuni ya Katani Limited zimesitisha uzalishaji tangu Agosti 21 ili kupisha maridhiano.

Kamati iliyoundwa na Shigela kufuatilia suala hilo ilibaini kasoro kwenye mfumo wa Siso hivyo kutoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi kabla uhusiano uliopo haujaendelea kwa manufaa ya pande zote mbili.

Serikali

Akiwa ziarani wilayani Mbinga mwanzoni mwa Januari, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imeamua kuboresha ufanisi katika mazao matano ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

“Mazao haya tutayasimamia kuanzia kilimo hadi uvunaji na utafutaji wa masoko. Nimeshafuatilia mazao ya korosho, tumbaku na pamba. Sasa nimeanza na kahawa na nimeamua kuanzia huku Mbinga,” alisema.

Kuhakikisha masilahi ya wakulima yanaimarishwa na mapato ya Serikali yanaongezeka aliagiza kahawa kuanza kuuzwa kwa mnada chini ya mfumo wa ushirika.

“Kuanzia msimu ujao, kahwa yote itauzwa kwa mnada, mnunuzi yeyote akitaka kununua aende mnadani, tukikukuta unanunua kwa mkulima tutakukamata,” alisema.

Majaliwa alitoa maagizo hayo baada ya kubaini madudu kwenye vyama vikuu vya ushirika vya Mbinga (Mbicu na Mbifacu) na kuagiza uchunguzi ufanyike.