Lijue tatizo la kukosa hedhi na namna ya kukabiliana nalo

Muktasari:

  • Nasema hivi kwa sababu, kibaiolojia hedhi ya kila mwezi, ni mchakato unaojiendesha wenyewe ndani ya mwili kwa ushirikiano wa mfumo wa homoni na mfumo wa uzazi pasipo ridhaa ya mwanamke mwenyewe, hivyo endapo mwanamke atashindwa kupata hedhi kikamilifu, ni ishara ya kuwa na tatizo aidha kwenye mfumo wa homoni au mfumo wa uzazi kwa ujumla wake ambako kuna sababishwa na matatizo mengine kama nitakavyoeleza.

Ni dhairi kuwa, kukosa au kutopata hedhi kabisa ni tatizo linalowapata wanawake wengi sana kwa siku za karibuni, na kutokana na maswali ya wasomaji wetu wa kila wiki nimeona leo nieleze ni nini hasa tatizo hili. Kwanza kabisa ifahamike kuwa, kukosa hedhi ni tatizo la kiafya hata kama lisiambatane na maumivu yeyote lakini mwanamke hapaswi kulifumbia macho tatizo hili.

Nasema hivi kwa sababu, kibaiolojia hedhi ya kila mwezi, ni mchakato unaojiendesha wenyewe ndani ya mwili kwa ushirikiano wa mfumo wa homoni na mfumo wa uzazi pasipo ridhaa ya mwanamke mwenyewe, hivyo endapo mwanamke atashindwa kupata hedhi kikamilifu, ni ishara ya kuwa na tatizo aidha kwenye mfumo wa homoni au mfumo wa uzazi kwa ujumla wake ambako kuna sababishwa na matatizo mengine kama nitakavyoeleza.

Tatizo hili kitaalamu linaitwa amenorrhea. Hii hutokea pale ambapo mwanamke anakosa kuona mzunguko wa hedhi kuanzia mwezi mmoja na kuendelea. Hivyo kwa mwanamke ambaye pia amekosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo, na kwa wasichana kuanzia miaka 15 hadi 18 ambao nao pia hawajaona mizunguko yao hedhi wapo kwenye kundi hili.

Sababu kubwa ya kukosa hedhi ambayo wengi tumeizoea ni ujauzito. Kwa tafsiri ya kawaida ujauzito ndiyo sababu ya asili ya kukosa hedhi. Kisayansi mwanamke hapati hedhi kabisa kwa kipindi chote cha ujauzito wake. Lakini tofauti na ujauzito, sababu nyingine ni pamoja na matatizo ya kiafya yanayojitokeza kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla na kwenye mfumo unaoratibu homoni mwilini na ni muhimu kuwaona wahudumu wa afya ili kuchunguza matatizo haya. Ni zipi hasa sababu zinazochangia tatizo hili? Wanawake wengi sana wamekuwa na swali hili kwangu. Tatizo la kutopata hedhi linatokea kwa sababu tofauti tofauti, baadhi yakisababishwa na aina fulani ya maisha ya mwanamke mwenyewe kwa kutumia aina fulani ya madawa, lakini pia uwepo wa matatizo mengine ya kiafya pia yanachangia tatizo hili.

Kwanza kabisa tatizo hili husababishwa na sababu za asili. Mwanamke anaweza kujikuta anakosa hedhi kutokana na sababu za asili kama vile ujauzito, mwanamke kufikia umri wa kupoteza uwezo wa kuzaa kutokana na sababu za kiumri lakini imethibitika hata kunyonyesha pia kunasababisha tatizo hili japo ni kwa wanawake wachache sana.

Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango. Mathalani, matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango, yanachangia kwa kiasi kikubwa sana kuharibu utendaji kazi wa mfumo wa homoni nakusababisha kukosa hedhi. Hivyo ni kawaida sana kwa baadhi ya wanawake wanaoutumia vidonge kama njia ya kupanga uzazi, kukosa hedhi kwa kipindi fulani. Hata baada ya kuacha kutumia vidonge hivyo, wanaweza kuchukua muda fulani ndipo wanaendelea kupata hedhi.

Baadhi ya matumizi ya dawa kwa ajili ya tiba ya magonjwa mengine pia yanachangia tatizo hili. Aina fulani ya madawa yamethibitika kua na uwezekano wa kuvuruga mfumo wa homoni na kusababisha kukosa hedhi kwa kipindi fulani. Dawa hizi ni pamoja na dawa za magonjwa ya akili, magonjwa ya saratani, sonona, dawa za shinikizo la damu na dawa za aleji. Hivyo ni kawaida kwa mwanamke aliye kwenye moja ya tiba hizi kukosa hedhi.

Lakini pia matatizo machache yanayojitokeza kwenye mfumo wa uzazi wenyewe pia yanachangia. Wakati mwingine ndani yanaota makovu ambayo yamejitokeza baada ya kufanyiwa upasuaji au tiba ya aina yeyote ili kuondoa vimbe zilizojitokeza kwenye mfuko wa uzazi. Sababu za kimuundo wa via vya uzazi pia zinachangia, mathalani kwa mwanamke ambae mlango wake wa kizazi ni mdogo na hauwezi kufunguka kuruhusu kutoka kwa damu, japo tatizo hili ni nadra sana kutokea.