Monday, July 9, 2018

MWISHO RUSSIA 2018: Ronaldo, Messi bado watia ngumu

 

MSHAMBULIAJI wa Ureno Cristiano Ronaldo, amelazimika kuwapandishia wale wanaomfuatafuata wakimtaka aseme kama atastaafu soka ya kimataifa baada ya Ureno kutupwa nje ya Fainali za Kombe la Dunia na Uruguay.

Mabingwa hao wa Ulaya walikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uruguay hatua ya mtoano na moja kwa moja Ronaldo na marafiki zake wakapaki mizigo yao na kuondoka Russia.

CRISTIANO RONALDO

Wakati baadhi ya mastaa wakitangaza kustaafu, ishu iko kwa Ronaldo aliyeisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Euro 2016 akiwa na Ureno, amekataa kuzungumzia hatma yake na akasema kwanza aachwe na wiki chache zijazo atatangaza msimamo wake.

Ronaldo mwenye miaka 34, fainali zijazo atakuwa na miaka 38 hivyo atakuwa na umri utakaomfanya ashindwe kunyumbulika uwanjani.

“Mbona mnanifuatafuata sana, huu si wakati wa kuzungumzia hatma yangu ila mjue tu, Ureno itaendelea kuwa timu bora, wachezaji bora, vijana, wenye mshikamano. Ninafuraha kusema timu hii ni wapambanaji na wanafanya makubwa.’

LIONEL MESSI

Machungu ya kutolewa Ronaldo ni sawa na hasimu wake, Lionel Messi ambaye yuko kimya hadi sasa. Argentina ilitolewa kibabe na Ufaransa kwa kuchapwa mabao 4-3 na Ufaransa ndani ya dakika 90.

Messi ameshacheza dakika 756 hatua ya mtoano, lakini hakuwahi kufunga. Baada ya filimbi ya mwisho, Messi aliinamisha kichwa chini lakini alipoulizwa kama atastaafu, hakutajka kusema moja kwa moja. Messi ana miaka 31 na fainali zijazo atakuwa na miaka 34.

Messi aliwahi kutangaza Juni 2016 kustaafu baada ya fainali za mwaka huu: “Nimejaribu katika fainali nne, nataka kombe, lakini kwa bahati mbaya haikuwa...”

GERALD PIQUE

Wakati Messi na Ronaldo wakikomaa, Gerard Pique amesema sasa basi kuitumikia timu ya taifa ya Hispania.

Hatua ya beki huyo wa Barcelona imekuja baada ya kupigwa kwa penalti 4-3 na Russia katika mechi iliyokuwa na ushindani. Hadi dakika 90 zinamalizika ngoma ilikuwa 1-1. Pique alisema: “Nimefurahi kuitumikia timu yangu, kila kitu chenye mwanzo kina mwisho, naona sasa niwapishe wengine...najivunia kuitumikia Hispania na kujivunia mafanikio na pengine kuna sababu nyingi, lakini naona sasa ni wakati wa kuwapisha wengine.”

Pique aliyekuwa aingie matatani kwa kudai uhuru wa Catalan alikuwa mhimili makini na beki mwenzake, Sergio Ramos katika kikosi cha Hispania.

JAVIER MASCHERANO, 3

Baada ya Argentina kuaga katika fainali za mwaka huu, beki mkongwe wa timu hiyo na Barcelona, Javier Mascherano ametangaza kuachana na soka ya kimataifa.

Mascherano alitangaza hatua hiyo baada ya Argentina kutandikw amabao 4-3 na Ufaransa katika mechi ya 16 Bora

Mcheaji huyo amecheza mechi zote nne mwaka huu lakini hata hivyo, alisema kuwa hiyo si sababu ya yeye kuendelea kung’ang’ania kubakia kwenye timu ambayo ameitumikia kwa zaidi ya miaka 10 sasa na fainali za Russia ni za nne kwake.

Hata hivyo, aliwaambia waandishi wa habari huko Kazan: “Ni wakati wangu wa kusema kwaherini na ninawakaribisha wengine.Katika soka huwezi kupata vitu unavyodhani unaweza kupata, na kitu cha msingi si kupingana na kila jambo.

“Tulikuwa na uwezo wa kila jambo, lakini tumeshindwa,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona na Liverpool anayekipiga China.

LUCAS BLIGIA

Nyota wa AC Milan, Lucas Biglia naye ametangaza kuachana na Argentina ‘La Albiceleste’.

“Soka ilivyo, kwa sasa tuna huzuni sana, kwa sababu baadhi yetu ndiyo tunamaliza. Nina imani watakaokuja kuchukua nafasi zetu, watafanya makubwa kwa Argentina kwa kila kinachostahiki,” Biglia aliiambia Fox Sports.

“Ni wakati wa mimi sasa kusema basi, kusema ukweli, kuna vijana wana vipaji wanastahili.”

ANDRES INIESTA

Aliifungia Hispania bao la ubingwa Fainali za 2010 ameshatangaza kuachana na soka la kimataifa baada ya kutolewa na Russia.

Iniesta 34, aliyeingia katika mchezo huo, alishuhudia timu yake ikilala kwa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti. Iniesta alikuwa wa kwanza kupiga na kufunga mkwaju wake wa mwisho kwa timu ya taifa, ilikuwa dakika ya 131.

“Ukweli hii ni mechi yangu ya mwisho na timu ya taifa,” alisema.

Iniesta, alianza kucheza timu ya taifa mwaka 2006, aliisaidia ukatika mechi za Ulaya na kutwaa ubingwa mwaka 2008 na 2012 wakati huo akiwa katika kiwango bora kabisa.

“Wakati mwingine kuachana na timu ya taifa kunatengena mengine mazuri zaidi kwa wengine,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona.

KEISUKE HONDA

Mashine nyingine ya Japan. Tayari ameshatangaza kuachana na soka ya kimataifa baada ya timu yake kuaga kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Mchezeshaji huyo,32, aliyewahi kukipiga AC Milan na CSKA Moscow anasema anataka kupisha wengine.

Anasema: “Nimemaliza soka yangu timu ya taifa.”Lakini nina furaha kwamba tuna vijana wengi wenye uwezo mkubwa, na ninaamini watafanya makubwa kwa Japan.

SARDAR AZMOUN

Azmoun ni kama ana hasira za timu yake ya Iran kufanya vibaya. Ametangaza kustaafu timu ya taifa akiwa na miaka 23 tu. Ana uwezo wa kucheza fainali mbili za Kombe la Dunia, za Qatar 2022 na Marekani 2026.

Mchezaji huyo wa klabu ya Rubin Kazan,23, alitangaza kupitia mtandao wake wa Instagram hataki tena timu ya taifa baada ya fainali za Russia.

Alisema kuwa kufanya vibaya kwa timu hiyo kumesababisha mama yake kuumwa na mara zote huumwa inapofungwa sasa alichofanya ni kustaafu mapema tu.

“Ninajivunia kuwakilisha timu ya taifa lakini kwa mazingira yaliyopo, ni wakati wa mimi kusema sasa basi,” aliandika kupitia akaunti yake ya Instagram.

MAKOTO HASEBE

Nahodha wa timu ya taifa ya Japan. Alitangaza kustaafu timu ya taifa baada ya kufanya ovyo Fainali za Russia. Ilifungwa mabao 3-2 na Ubelgiji na kuaga fainali hizo.

“Nimeamua kuachana na soka la kimataifa kupitia fainali hizi,” Hasebe aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.

Kiungo huyo mkabaji anaachana na Blue Samurai alisema kuwa wakati umefika kwa wengine kuonyesha vipaji vyao.

-->