Mataifa ya Ulaya na uzalendo wa lugha zao

Muktasari:

  • Katika makala haya tutatoa mifano ya jitihada zinazofanywa na mataifa ya Uingereza na Ujerumani, kuonyesha namna wanavyozithamini lugha zao.

Kutokana na ukweli kwamba lugha ndio kinywa cha utamaduni wa jamii yoyote iwayo, mataifa ya kigeni yanafanya kila aina ya jitihada kuenzi lugha zao.

Katika makala haya tutatoa mifano ya jitihada zinazofanywa na mataifa ya Uingereza na Ujerumani, kuonyesha namna wanavyozithamini lugha zao.

Kama inavyofahamika, Kiingereza kinatumiwa na mataifa mengi ulimwenguni katika matumizi mbalimbali.

Miongoni mwa matumizi hayo ni yale muhimu kabisa ya kitaaluma. Mataifa yanayotumia Kiingereza yangeweza kutumia lugha zake yenyewe. Uingereza kwa kulitambua hilo na kwa mikakati yake inazisaidia nchi hizo kwa namna mbalimbali, ikiwamo kutoa ufadhili wa zana mbalimbali za kitaaluma.

Pamoja na kufanya hivyo, taifa hilo hutoa udhamini wa kimasomo katika ngazi mbalimbali za elimu. Yote hayo hufanyika kwa malengo maalumu ya kukienzi Kiingereza ili kiendelee kuwa lugha ya dunia.

Halikadhalika nchini Ujerumani, ingawa kwa kulinganisha na Kiingereza, Kijerumani hutumika zaidi nchini humo; Wajerumani wana mapenzi makubwa na lugha yao kuliko lugha nyingine hususan katika mawasiliano, kazi na elimu.

Tofauti na hivyo, wanajifunza lugha nyingine za kigeni kwa ajili ya shughuli maalumu za kitaaluma, utalii na kadhalika.

Nchini Ujerumani, katika mawasiliano ya kawaida, ya kikazi na shughuli nyinginezo, Kijerumani hupewa kipaumbele. Hata kama katika mawasiliano yafahamika kwamba mtu fulani si Mjerumani lakini kwa kuwa anawasiliana na Mjerumani, Kijerumani kitatumika mpaka mhusika aseme kwamba haijui lugha hiyo.

Aidha, mgeni ambaye hakijui Kijerumani anapotaka kupata maelekezo fulani kwa mwenyeji kwa kutumia lugha mathalani ya Kiingereza, baadhi ya wenyeji hao hujinadi kwamba hawajui Kiingereza (hata kama wanakijua).

Katika taaluma ya utamaduni na lugha tafsiri yake ni kwamba Wajerumani wana uzalendo mkubwa na utamaduni na lugha yao. Halikadhalika, kama tulivyoona kwa Waingereza.

Hali ilivyo kwa Waswahili

Katika mazingira yetu Waswahili, kuna udhaifu mkubwa. Wengi hatuna uzalendo na lugha yetu.

Baadhi ya watumiaji wazawa wa Kiswahili wanapokutana na wageni, yaani watu wa kutoka mabara ya Ulaya, Asia, Amerika na kwingineko huwapapatikia kwa kuongea Kiingereza hata kama ni Kiingereza kibovu isivyomithilika!

Wengi wetu hufanya hivyo wakidhani kwamba kila ‘mtu mweupe’ anajua Kiingereza. Matokeo yake baadhi ya wageni hao hubaki wakitushangaa.

Matarajio yao ni kwamba wanapowasili nchini Tanzania kwa mfano, watawasikia Watanzania wakijidai na Kiswahili chao ili nao kama watalii waweze kujifunza au kuboresha Kiswahili kidogo wanachokifahamu ambacho wamejifunza kwa malengo ya kitalii, ili kurahisisha mawasiliano wawapo katika nchi zinazotumia Kiswahili.

Baadhi ya wasomi pia wana mtazamo potofu kabisa dhidi ya lugha ya Kiswahili. Kwa sababu hiyo katika mazingira mbalimbali hukibeza Kiswahili kwa maneno na matendo yao, kiasi cha kuwaambukiza wasio wasomi mtazamo huo mufilisi wa kikasumba.

Ukweli ni kwamba Kiswahili ndiyo lugha yetu na lugha za kigeni ni za wenyewe. Kwa maelezo hayo hatumaanishi kwamba tusitaalamikie lugha za kigeni, la hasha!

Tujifunze lugha nyingi za kigeni tuwezavyo na kuzitumia katika mazingira yanayotakiwa lakini Kiswahili chetu kiwe ‘nambari wani’ katika mazingira yetu.

Kwa kufanya hivyo tutakienzi, kukikuza na kukitangaza mbele ya mataifa. Itawalazimu pia wageni wajifunze Kiswahili ili waweze kuwasiliana na Waswahili kama wageni wawapo katika mataifa ya Ulaya wanavyolazimika kujifunza lugha za Ulaya ili kukidhi haja ya mawasiliano.